Sep 30, 2022 01:23 UTC
  • Sheikh Issa Qassim: Muqawama ni wenzo wa kukabiliana na njama za maadui wa Uislamu na Waislamu

Sheikh Issa Qassim, kiongozi wa kimaanawi wa mapinduzi ya Bahrain amesema kuwa, kuna haja ya kudumisha njia ya muqawama na mapambano katika eneo la Asia Magharibi kama wenzo wa kukabiliana na hujuma na njama za mabeberu.

Ayatullah Issa Qassim amesisitiza kuwa, muqawama na mapambano ndiyo chaguo pekee la kukabiliana na njama na mipango michafu ya maadui wa Uislamu na Waislamu.

Kiongozi huyo wa kimaanawi wa mapinduzi ya Bahrain kadhalika ameeleza kwamba, njama za maadui wa Uislamu pamoja na vibaraka wao wanaotaka kutoa pigo kwa dini ya Uislamu na wafuasi wake zitakwama na kushindwa kufikia malengo yake kwa kudumishwa muqawama na mapambano ya wananchi.

Katika ujumbe wake aliouandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Sheikh Issa Qassim amelaani vikali sera na siasa za utawala wa kifalme wa Bahrain za kuwakandamiza wananchi wanaopigania mageuzi na demokrasia.

Maandamano ya wananchi wa Bahrain

 

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hivi karibuni Kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Bahrain alikosoa vikali uamuzi wa utawala wa Aal Khalifa wa kuanzisha kitongoji cha walowezi wa Kiyahudi katika mji mkuu Manama na kueleza kwamba, hatua hiyo ni jinai na dhulma ya wazi dhidi ya wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Radiamali hiyo ya Sheikh Issa Qassim ilifuatia kutangazwa mpango wa utawala wa Aal Khalifa wa kubadilisha kwa takribani asilimia 40 ya vitongoji vya kale katika mji wa Manama na kuvipa nembo na utambulisho wa Kiyahudi.

Tayari hivi sasa kuna ununuzi usiokoma wa majengo hayo ya kale tena kwa bei ya juu lengo likiwa ni kulibadilisha eneo hilo baadaye na kulifanya kuwa kitongoji cha walowezi wa Kiyahudi.