Sep 30, 2022 01:24 UTC
  • Walowezi wa Kiyahudi wandelea na hujuma na uvamizi wao dhidi ya msikiti wa al-Aqswa

Kundi kubwa la walowezi wa Kiyahudi likisaidiwa na vikosi vya usalama vya utawala ghasibu wa Israel limeuvamia msikiti mtakatifu wa al-Aqswa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Duru za Palestina zinaripoti kuwa, katika muendelezo wa hujuma na vitendo vya chuki vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina, mamia ya walowezi wa Kiyahudi wamevamia tena msikiti mtakatifu wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu na kufanya vitendo vya kichochezi na vya kulivunjia heshima eneo hilo takatifu.

Tangu Jumatatu iliyopita walowezi wa Kiyahudi wameshadidisha hujuma na uvamizi wao dhidi ya msikiti wa al-Aqswa kwa kisingizio cha kuanza mwaka mpya wa Kiyahudi.

Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika Msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.

 

Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.

Asasi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa na baraza lake la usalama zinakosolewa na kulaumiwa kutokana na kutochukua hatua za maana za kukabiliana na hatua mbalimbali zisizo za kibinadamu zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel huko Palestina sambamba na uvamii wa mara kwa mara wa walowezi wa Kiyahudi dhidi ya msikiti wa al-Aqswa.

Tags