Sep 30, 2022 07:26 UTC
  • Al-Halbousi: Uthabiti wa Iraq si kipaumbele cha Marekani kwa sasa

Spika wa bunge la Iraq amesema, uungaji mkono wa Marekani kwa Iraq zaidi ni wa vyombo vya habari kuliko wa kiuhalisia na kwamba uthabiti wa Iraq si kipaumbele cha Washington kwa sasa.

Baada ya kupita takriban miezi miwili, kikao cha Bunge la Iraq kilifanyika siku ya Jumatano na wajumbe wa Bunge hilo hawakukubali kujiuzulu kwa Spika Mohammad Al-Halbousi, na hivyo Al-Halbousi akabaki katika nafasi ya Uspika wa Bunge la nchi hiyo.
Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Al-Arabiya, Spika wa Bunge la Iraq amesema: mazungumzo ya kuunda serikali ya nchi hiyo yalianza siku chache zilizopita, na kwamba, muungano wa pande tatu za al-Siyadah, Chama cha Kidemokrasia cha Kurdistan na mrengo wa Sadr umehitimisha suala la wabunge wa mrengo wa Sadr kujiondoa bungeni.
Bunge la Iraq

Al-Halbousi amebainisha kuwa, hakuna anayeweza kuipuuza harakati ya Sadr na kusisitizia umuhimu wa kuanza tena vikao vya bunge; na akasema, kujiuzulu kwake ni suala la binafsi na kwamba ni jambo la lazima kuwepo mrengo tawala na mrengo wa upinzani nchini humo.

Pamoja na hayo, Spika wa Bunge la Iraq amesema: inapasa pande zote zianze mazungumzo bila kuwekeana masharti na kutozihamishia nje ya bunge tofauti zao za kisiasa.
Uchaguzi wa mapema wa bunge la Iraq ulifanyika Oktoba 10, 2021, lakini licha ya kupita miezi 11 tangu ulipofanyika uchaguzi huo, hadi sasa makundi, vyama vya siasa pamoja na mirengo iliyoko bungeni haijaweza kuunda serikali mpya kutokana na tofauti za kisiasa zilizoko baina yao.../

 

Tags