Sep 30, 2022 11:52 UTC
  • Hamas: Jinai za Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina ni ukatili

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imekashifu jinai za Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina na kusema zinatokana na tabia ya ukatili wa “kisadism".

Kauli hiyo ya Hamas imetolewa kufuatia mauaji ya kikatili ya mtoto wa Kipalestina mikononi mwa askari wa utawala wa Israel.

Rayyan Yaser Suleiman aliyekuwa na umri wa miaka saba alifariki dunia katika mji wa Taquu karibu na mji wa Bait Laham katika sehemu ya kusini ya Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel mapema jana Alhamisi. Rayyan alipoteza maisha wakati yeye na wanafunzi wenzake walipokuwa wakikimbizwa vikali na wanajeshi wa Israeli walipokuwa wakirudi nyumbani kutoka shuleni.

Taarifa ya Wizara ya Afya ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina yenye makao yake Ukingo wa Magharibi imesema, mtoto huyo alifariki dunia baada ya kuanguka kutoka mahali pa juu wakati alipokuwa akikimbizwa na wanajeshi wa Israel waliokuwa wamejizatiti kwa silaha.

Ikizungumzia tukio hilo, Hamas imesisitiza kwamba "uhalifu wa jeshi la Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina, watu, ardhi na matukufu yao hautaipatia Israeli usalama."

Taarifa ya Hamas imeongeza kuwa, ukatili huo mbaya, unazidisha nguvu ya muqawama na mapambano ya Palestina ya kutetea ardhi na haki za Wapalestina hadi Palestina itakapokombolewa kikamilifu."

Likiwanukuu wahudumu wa afya katika Hospitali ya Serikali ya Beit Jala, ambapo Rayyan alitangazwa kuwa amefariki dunia, shirika rasmi la habari la Wafa la Palestina limesema, mapigo ya moyo wa mtoto huyo yalisimama alipokuwa akikimbizwa na wanajeshi wa Israel.