Sep 30, 2022 12:37 UTC
  • Mkwamo mpya wa kisiasa Lebanon baada ya Bunge kushindwa kumchagua Rais

Kikao cha kwanza cha Bunge la Lebanon kilichoitishwa kwa ajili ya kumchagua Rais mpya wa nchi hiyo kilimalizika Alkhamisi ya jana bila ya kuwa na natija.

Kipindi cha uongozi wa miaka 6 cha Rais wa sasa Michel Aoun kinamalizika tarehe 31 ya mwezi ujao wa Oktoba. Bunge la Lebanon linapaswa kumchagua Rais mpya mwezi mmoja kabla ya kumalizika kipindi cha uongozi wa Rais aliyeko madarakani. Bunge la Lebanon lina Wabunge 128 na ili mgombea wa kiti cha urais atangazwe kuwa mshindi anapaswa kupata theluthi mbili ya kura. Aidha kwa mujibu wa katiba, Rais wa nchi anapaswa kuchaguliwa kutoka miongoni mwa Wakristo wa Kimaroni. Kufanyika kikao cha kwanza cha Bunge la Lebanon kunabeba risala na jumbe mbili muhimu.

Ujumbe wa kwanza; ni idadi ya Wabunge waliohudhuria kikao cha kwanza cha Bunge hilo. Wabunge 122 kati ya Wabunge wote 128 wa Bunge la Lebanon walihudhuria kikao cha jana na kushiriki katika zoezi la upigaji kura. Mahudhurio ya idadi hii kubwa ya Wabunge katika kikao hicho ni ithbati tosha kwamba, makundi na mirengo ya kisiasa nchini humo yanakipa umuhimu cheo cha urais.

Ujumbe mwingine ni kwamba, kuna hitilafu nyingi baina ya makundi na mirengo ya kisiasa nchini Lebanon kuhusiana na nani anayepaswa kuwa rais mpya ambaye atarithi mikoba ya Rais Michel Aoun anayemaliza muda wake. Wabunge 63 kati ya Wabunge 122 waliohudhuria kikao cha jana walirejesha karatasi za kura zikiwa nyeupe na hawakuwa tayari kumpigia kura mgombea yeyote kati ya wagombea waliojitokeza kuwania kiti hicho.

Michel Moawad, mgombea kiti cha Urais Lebanon ambaye hakupata kura za kumuwezesha kutangazwa Rais

 

Michel Moawad alishika nafasi ya kwanza katika kinyang'anyiro hicho akipata kura 36  kati ya 122 za Wabunge waliohudhuria kikao hicho huku Salim Edde akiambulia kura 11 na kura 12 zikibatilika. Inaonekana kuwa, sababu kuu ya Wabunge 63 kurejesha karatasi zao za kupigia kura zikiwa nyeupe inarejea katika mchakato wa kuarifishwa wagombea ambao mfungamano wao ni nje ya Lebanon. Sayyid Hashim Safiuddin, Mkuu wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon amesema kuwa, baadhi wanakosea, kwani kila kunapokuweko uchaguzi au mpango wa kuiokoa Lebanon wao hufuatilia suala la kudhamini maslahi ya Marekani.

Hizbullah haitaruhusu na haikubali wananchi wa Lebanon kutwishwa Rais ambaye atakuwa kigaragosi na mwanasesere wa dola vamizi na la kibeberu la Marekani.

Wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, baada ya kikao cha kwanza cha Bunge kushindwa kumchagua Rais hapo jana, inaonekana kuwa, Lebanon inajongewa na mkwamo mpya wa kisiasa. Uchaguzi wa Bunge ulifanyika Mei mwaka huu na Najib Mikati akateuliwa kuwa Waziri Mkuu na kupewa jukumu la kuunda serikali. Hata hivyo imepita miezi minne na hadi sasa hajafanikiwa kuunda serikali mpya. Hitilafu na mizozo baina ya Rais Michel Aoun na Waziri Mkuu Najib Mikati inatajwa kuwa sababu na kiini halisi cha kutoundwa hadi sasa serikali mpya ya nchi hiyo.

Michel Aoun, Rais wa Lebanon anayemaliza muda wake

 

Filihali wakati Lebanon kwa miezi kadhaa sasa inakabwa na jinamizi la kushindwa kuunda Baraza la Mawaziri, huenda ikatumbukia katika mgogoro mwingine mpya wa kushindwa kumchagua Rais. Hii ni katika hali ambayo, baada ya kikao cha kwanza cha Bunge, hakujatangazwa tarehe nyingine ya kufanyika uchaguzi huo.

Nukta ya mwisho ni hii kwamba, kutumbukia Lebanon katika mkwamo wa kushindwa kumchagua Rais mpya kunaweza kuifanya anga ya kisiasa ya nchi hiyo kuzidi kuwa tete sambamba na kuongeza matatyzo ya kiuchumi ambayo tayari yanaiandama nchi hiyo hivi sasa. Ni kwa muktadha huo, ndio maana Nabih Berri Spika mkongwe wa Bunge la Lebanon akasisitizia udharura wa kuchaguliwa Rais mpya na kubainisha kwamba, kuchaguliwa Rais mpya katika wakati ulioainishwa ni jambo ambalo lina udharura maradufu.