Oct 01, 2022 04:04 UTC
  • Indhari ya Umoja wa Mataifa kwa wanamgambo wa Taliban

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Afghanistan (UNAMA) amekosoa vikali hatua ya wanamgambo wa Taliban wanaotawala nchini humo ya kutochukua hatua kuboresha haki za watu katika nchi hiyo hususan ya mabanati na wanawake na kuonya kuwa, yamkini subira ya jamii ya kimataiifa kuhusiana na utendaji wa wanamgambo hao ikafikia kikomo.

Markus Potzel, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Afghanistan amesema hayo katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Afghanistan na kueleza kwamba, mibinyo inayoongezeka dhidi ya haki za wanawake inaonyesha kuwa, kundi la Taliban linapuuza jamii ya watu wanaounda zaidi ya asilimia 50 nchini Afghanistan, na inaonekana kuwa kundi hilo linataka kukabiliwa na hatari ya kutengwa kimataifa.

Potzel ameongeza kuwa, yamkini subira ya akthari ya wajumbe wa jumuiya za kimataifa kuhusiana na mkakati wa kuamiliana na Taliban ikafikia tamati.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amekumbusha kuwa, katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, kumeshuhudiwa mabadiliko machache sana ambayo ni chanya huku matukio hasi yakiwa mengi.

Hatua ya kundi la wanamgambo wa Taliban ya kutotekeleza ahadi zake katika masuala mbalimbali likiwemo suala la kuheshimu haki za mtu binafasi na za kijamii za wanawake hususan haki yao ya kusoma na kufanya kazi sambamba na kuunda serikali jumuishi, ni miongoni mwa masuala ambayo yanaifanya jamii ya kimataifa  ielekeze ukosojia wake kwa serikali ya Taliban ambayo iko madarakani kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Mabinti wa Afghanistan ambao wanakosa fursa ya kwenda shule kutokana na sera za serikali ya wanamgambo wa Taliban

 

Katika miezi ya hivi karibuni serikali ya Taliban imetoa ahadi mara kadhaa kwamba, itatambua rasmi haki za wanawake nchini Afghanistan na kuandaa mazingira ya mabinti na wanawake kusoma na kufanya kazi. Tangu wanamgambo wa Taliban waliposhika tena hatamu za uongozi nchini Afghanistan Agosti mwaka jana, shule za wasichana zimefungwa na hivyo kupelekea maelfu ya wanafunzi wa kike katika majimbo mbalimbali ya nchi hiyo kukosa fursa ya kuendelea na masomo.

Jamii ya kimataifa imetangaza na kuweka wazi na bayana kwamba, moja ya vigezo muhimu kabisa vya kuitambua rasmi serikali ya Taliban nchini Afghanistan ni kuunda serikali jumuishi na kuheshimu haki na uhuru wa wanawake na kwamba, kuendelea siasa za kuibanabana jamii ya wanawake ni jambo ambalo litapelekea kuongezeka hali ya kutokuwa na imani na Taliban, na hivyo kuweko azma zaidi ya kutoshirikiana na kundi hilo.

Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Afghanistan akatahadharisha kwamba, yumkini subira ya jamii ya kimataifa kuhusiana na kushirikianan na kundi la Taliban ikafikia tamati. Kutokana na Taliban kutotekeleza ahadi zake na majukumu yake mkabala na wananchi wa Afghanistan, filihali kuna mtazamo huu kwamba, kuendelea mwenendo huu kutapelekea kuongezeka mibinyo ya kiuchumi dhidi ya nchi hiyo. Katika mazingira kama haya, misaada ya kimataifa kwa Afghanistan nayo kinyume na matarajio ya Taliban itapungua siku baada ya siku.

Njaa nchini Afghanistan inatishia uhai wa mamilioni ya watu

 

Sayyid Jawad Husseini mweledi wa masuala ya kisiasa nchini Afghanistan anasema: Madhali serikali ya Taliban haijatoa majibu chanya kwa matakwa ya jamii ya kimataifa, sidhani kama jamiii ya kimataifa itakuwa tayari kuutambua rasmi utawala wa wanamgamno hao.

Hali ya kiuchumi nchini Afghanistan hivi sasa ni mbaya kuliko hapo kabla. Hii imetokana na hatua ya serikali ya Marekani kuendelea na msimamo wake wa kuzuia fedha za Benki Kuu ya Afghanistan na wakati huo huo kung'ang'ania Taliban kuendeleza siasa zake za mbinyo dhidi ya makundi mbalimbali ya kiraia jambo ambalo litapelekea kusimamishwa misaada ya kimataifa na kutotambuliwa rasmi serikali ya kundi hilo.

Ripoti ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) inaonyesha kuwa, watu milioni 24.4 nchini Afghanistan miongoni mwao watoto milionii 13 wanahitajia misaada ya kibinadamu, huku raia milioni 18 wa nchi hiyo wakikabiliwa na hali ya dharura au mgogoro wa kushindwa kujidhaminia mahitaji ya chakula ambapo kuna watoto zaidi ya milioni moja katika orodha hiyo.

Hii ni katika hali ambayo, mwaka uliopita (2021) watu wapatao milioni saba walibakia bila makazi nchini Afghanistan. Shirika la Save The Children limetahadharisha katika ripoti yake kwamba, endapo misaada ya harakka haitapelekwa nchini Afghanistan basi mamilioni ya watu watapoteza maisha nchini humo kwa baa la njaa.

Kwa kuzingatia indhari za mara kwa mara za kimataifa kuhusianan na matokeo mabaya ya kuendelea hali ya sasa nchini Afghanistan yaani kuendelea hatua ya serikali ya Marekani ya kuzuia fedha za kigeni za Benki Kuu ya Afghanistan na wakati huo huo kung'ang'ania Taliban kutobadiliisha utendajii wake, pande zote hizi mbili zinawajibika na maafa tarajiwa ya kibinadamu nchini Afghanistan.

Tags