Oct 02, 2022 08:13 UTC
  • Matokeo ya kustaajabisha ya uchaguzi wa Bunge la Kuwait, wafungwa watoka jela waingia Bungeni

Matokeo ya uchaguzi wa Bunge la Kuwait yamewashangaza wengi. Wapinzani wamepata viti vingi, nafasi ya Waislamu wa madhehebu ya Kishia nayo imeimarika kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea na wafungwa wawili wametoka jela na kuingia bungeni.

Baraza la Shura ya Taifa (Bunge la Kuwait) lilianzishwa tarehe 23 Januari 1963. Uchaguzi wa karibuni kabisa wa Bunge la Kuwait ni ule uliofanyika Alkhamisi ya tarehe 29 Septemba katika majimbo matano ya uchaguzi. Uchaguzi huo ulikuwa wa 17 wa Bunge la Kuwait na wa pili tangu alipoingia madarakani Amir wa hivi sasa wa nchi hiyo, Nawaf al-Ahmad al-Jaber al-Sabah. Nawaf al-Sabah aliingia madaraka mwezi Septemba 2020 huko Kuwait.

Kipindi cha kila Bunge nchini Kuwait ni miaka minne. Lakini Bunge lililopita lililoanza mwezi Disemba 2020 yaani miezi mitatu tu tangu kuingia madarakani Amir mpya, Nawaf al-Sabah, limehudumu kwa muda wa miezi 20 tu kabla ya kufunjwa na Amir huyo kutokana na mzozo uliotokea baina ya Bunge na Serikali.

Bunge la Kuwait

 

Tofauti na mabunge ya nchi nyingine za Kiarabu, Bunge la Kuwait lina nguvu na taathira katika maamuzi ya nchi. Bunge la Kuwait lina nguvu za kutunga sheria na kusimamia vilivyo sheria hizo kiasi kwamba kila mbunge ana nguvu za kikatiba za kumwita bungeni Waziri Mkuu au waziri yeyote wa serikali kwa ajili ya kusailiwa. Muswada wa kumwita Waziri Mkuu au waziri yeyote yule wa serikali hufikishwa kwa Amir wa Kuwait na kuna uwezekano wakati huo hata baraza zima la mawaziri likavunjwa. Kiujumla Bunge la Kuwait lina umuhimu mkubwa katika muundo wa utawala wa nchi hiyo.

Katika uchaguzi wa siku ya Alkhamisi ya tarehe 29 Septemba, wagombea 313 walichuana kwenye majimbo matano wakiwemo wanawake 22 kwa ajili ya kuwania viti 50 vya Bunge. Watu laki saba na 95,920 ndio waliotimiza masharti ya kupiga kura. Televisheni ya al Jazeera ya Qatar ilitoa uchambuzi kuhusu matokeo ya uchaguzi wa bunge hilo na kusema kuwa matokeo hayo hayakutarajiwa, ni ya kustaajabisha na ni ya kushangaza katika pande kadhaa. 

Watu wa hali mbalimbali wameshiriki katika uchaguzi

 

Mosi: Wapinzani wamepata asilimia 60 ya viti bungeni na wabunge 30 wa kambi hiyo ya upinzani wameingia bungeni akiwemo Ahmmad al Saadoun, Spika wa zamani wa Bunge la Kuwait.

Pili: Waislamu wa madhehebu ya Kishia wamefanikiwa kupata viti 10; ushindi ambao haujawahi kushuhudiwa katika historia ya Kuwait. Katika chaguzi za mabunge ya 15 na 16 ya Kuwait, Mashia walipata viti sita tu vya Bunge.

Tatu: Wagombea wawili waliokuwa wamefungwa kwa ajili ya kutumikia kifungo vha miaka miwili jela wameshinda katika uchaguzi na hivyo wametoka jela na kuingia bungeni.

Nne: Wanawake ambao katika bunge lililopita hawakupata hata kiti kimoja, mara hii wamepata viti viwili.

Tano: Ni wabunge wawili tu wa mrengo wa Kisalafi ndio waliofanikiwa kuingia bungeni katika uchaguzi huo mpya.

Na Sita: Ni wabunge 23 tu wa bunge lililopita ndio walioweza kutetea viti vyao na wabunge 27 waliobakia, wote ni wapya.

Wanawake wamepeleka wawakilishi wawili katika Bunge la Kuwait wakati katika bunge lililopita hakukuwa na hata mbunge mmoja mwanamke

 

Pamoja na hayo yote, lakini kuna mambo yanayofanana baina ya bunge hili jipya na bunge lililopita. Bunge lililopita lilikuwa na mabadiliko ya asilimia 60 kuliko la kabla yake yaani Bunge la 15. Hivi sasa bunge hili la 17 limekuwa na asilimia 54 ya mabadiliko ikilinganishwa na Bunge la 16. Hayo ni mabadiliko ambayo bila ya shaka yoyote yataathiri mno maamuzi ya Bunge. Matokeo ya uchaguzi wa Bunge wa tarehe 29 Septemba 2022 kwa mara nyingine yameonesha kuwa, muundo wa utawala wa Kuwait hauingilii mchakato wa uchaguzi na unatoa uhuru kwa wananchi kujichagulia wenyewe wabunge wao.

Lakini pia tangu hivi sasa tunaweza kutabiri kuwa, Bunge hili jipya nalo halitoweza kumaliza miaka minne ya umri wake kutokana na muundo wa wabunge wake. Ni vyema tuseme pia hapa kwamba, Kuwait ni katika nchi zenye utulivu zaidi kati ya nchi za Kiarabu za Asia Magharibi na matokeo ya uchaguzi wa Bunge hayapunguzi kivyovyote vile nguvu za wananchi na serikali yao.