Oct 03, 2022 09:19 UTC
  • Ujerumani yachochea vita dhidi ya Yemen kwa kuiuzia Saudia silaha

Takriban wiki moja baada ya ziara ya Kansela wa Ujerumani Olaf Schultz nchini Saudi Arabia, Berlin kwa mara nyingine tena imeanza kuiuzia Saudia Arabia silaha na zana za kivita.

Tangu mwishoni mwa mwaka 2018, Ujerumani ilitangaza kuwa imeiwekea Riyadh vikwazo vya silaha, kwanza kwa kupinga uingiliaji wa Saudi Arabia katika vita vya Yemen na kisha kwa sababu ya mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari wa Kisaudi. Lakini sasa Berlin imeanzisha tena rasmi mauzo ya silaha kwa Saudi Arabia, huku muungano vamizi wa nchi hiyo ukiendelea kutumia silaha na zana hizo katika vita dhidi ya watu wasio na hatia wa Yemen.

Undumakuwili wa sera na vitendo vya serikali ya sasa ya Ujerumani katika suala hilo umewakasirisha raia na viongozi wengi wa kisiasa.

Sevim Dağdelen mjumbe wa Tume ya Sera za Kigeni ya Bunge la Shirikisho la Ujerumani kutoka Chama cha Mrengo wa Kushoto (die Linke), anasema kuhusiana na kadhia hiyoo kwamba: Mpango huu unafichua ukweli wa sera ya kigeni ya serikali ya mseto inayodai kuheshimu maadili, ambayo imesafisha uso wa Mohammad bin Salman, muuaji wa Khashoggi. Mohammed bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, anaongoza vita vya mauaji dhidi ya raia wa Yemen na kukandamiza upinzani wowote ndani ya Saudi Arabia.

Kansela wa Ujerumani Olaf Schultz akiwa na Mohammad bin Salman nchini Saudia

Kuuza silaha ni mojawapo ya sera kuu za kiuchumi na kisiasa za nchi za Magharibi, ambazo kupitia mauzo ya silaha hizo hupata mabilioni ya dola kila mwaka. Silaha hizo zinauziwa zaidi nchi ambazo zimo katika orodha ya wavunjaji wa haki za binadamu, hivyo katika miaka ya hivi karibuni na kwa kuendelea vita vya kidhalimu vya Saudia dhidi ya Yemen, Riyadh imekuwa miongoni mwa wanunuzi wakubwa wa silaha kutoka nchi za Ulaya. Kwa hakika, ijapokuwa nchi za Ulaya na Marekani zinapiga kelele kupitia kaulimbiu zenye hadaa za eti kupinga vita na kuzungumzia amani, lakini kiuhalisia zinashiriki katika jinai za kivita za nchi kama vile Saudi Arabia zilizo na mikataba mikubwa ya silaha na nchi hizo.

Janine Whistler, mwanachama mwandamizi wa Chama cha Kushoto  cha Ujerumani, anasema kuhusiana na hilo: "Kuiuzia silaha nchi ambayo inakiuka haki za wanawake na binadamu, kumuua Jamal Khashoggi na kuanzisha vita vya jinai dhidi ya Yemen ni kashfa."

Katika miaka ya hivi karibuni, kuakisiwa jinai za muungano wa Saudia huko Yemen na mauaji ya wanawake na watoto katika nchi hiyo kumezusha wimbi la hasira, chuki na maandamano ya umma dhidi ya siasa za serikali za Magharibi. Wananchi katika nchi za Magharibu wanataka serikali zao ziache kuziuzia silaha nchi kama Saudi Arabia ambazo zinakiuka wazi haki za binadamu.

Watoto ni wahanga wakuu wa vita vya Saudia dhidi ya Yemen

Inaelekea kuwa msimamo wa nchi za Magharibi umebadilika kuhusu kuiuzia Saudi Arabia silaha. Kwa hakika, vita kati ya Russia na Ukraine na ukosefu wa nishati umezifanya nchi za Magharibi kubadilisha mtazamo wao kuelekea Saudi Arabia. Ujerumani imetangaza baada ya ziara ya Schultz mjini Riyadh, kuwa inataka kurekebisha uhusiano wake na Riyadh ili kupata ushirikiano wa nchi hiyo katika kuwapa Wajerumani mafuta na gesi. Katika safari hiyo pia ametia saini makubaliano ya kununua meli inayobeba gesi ya LNG kutoka Qatar ambayo shehena yake inatakiwa kuwasili nchini Ujerumani mwishoni mwa Disemba mwaka huu.

Kwa hakika, ijapokuwa nchi za Magharibi zinatoa kaulimbiu za kupinga vita na kuzungumzia amani, kivitendo, sio tu kwamba hazizingatii kaulimbiu zozote, bali pia zinaanzisha au kuchochea vita katika sehemu zote za dunia. Wakati huo huo, watu wa nchi zilizokumbwa na vita ndio wahanga wakuu wa sera hizo za kibepari za Magharibi za kupata faida kubwa katika mauzo ya silaha.

 

Tags