Oct 04, 2022 06:19 UTC
  • Lebanon na Israel zakaribia kufikia makubaliano ya kuweka mipaka ya baharini

Taarifa zinaonyesha kuwa rasimu ya mwisho iliyopokelewa kutoka upande wa Marekani kuhusu kuainisha mipaka ya bahari ya Lebanon na utawala wa Kizayuni wa Israel itapelekea kupunguzwa tofauti kati ya pande hizo mbili.

Lebanon na utawala wa Kizayuni zinazozana kuhusu eneo la kilomitamraba 860 katika Bahari ya Mediterania ambalo lina rasilimali ya mafuta na gesi. Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Beirut na Tel Aviv yalianza Oktoba 2020 chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kuamua mipaka ya baharini kati ya pande hizo mbili, na raundi tano zilifanyika, ya mwisho ikiwa Mei 2021. Hata hivyo, mazungumzo hayo yalisitishwa Mei 2021 kutokana na mzozo kuhusu eneo linalozozaniwa na pia kufuatia ombi la pande zote mbili.

Wakati wa mazungumzo ya awali, Lebanon ilisisitiza haki yake ya kupanua ufikiaji wa maji ya Mediterania kuelekea kusini na kuongeza ufikiaji huo kutoka kilomitamraba 860 hadi kilomitamraba 2,300. Baada ya mzozo huo, Amos Hochstein, mshauri mkuu wa Marekani kuhusu usalama wa nishati duniani, alichaguliwa kuwa mpatanishi wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Lebanon na Israel na kujaribu kupunguza mzozo kati ya pande hizo mbili.

Zaidi ya mwaka mmoja baada ya mazungumzo hayo kusitishwa, Israel ilituma meli ya Ugiriki kwenye maji ya eneo la gesi ya Karish, ambayo Lebanon inaamini iko katika maji yanayozozaniwa kati ya pande hizo mbili, na hivyo Israel haina haki ya kuchimba mafuta au gesi katika eneo hilo hadi makubaliano yafikiwe. Kwa msingi huo, Seyyed Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon alitoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni kuhusiana na suala hilo.

Meli ikiwa katika eneo la machimbo ya gesi katika Bahari ya Mediterenia

Akizungumzia kuwasili kwa meli hiyo katika eneo la Karish, Seyed Hassan Nasrallah alisema kuwa suluhisho la kadhia hiyo linaweza kufikiwa kupitia mazungumzo na iwapo hilo haliwezekani basi kutakuwa na suluhisho la kivita.

Sambamba na kuwasili mjumbe maalumu wa Marekani wa upatanishi kati ya Beirut na Tel Aviv, Hizbullah ya Lebanon ilitoa onyo kali kwa meli za utafiti wa mafuta na gesi zilizokodiwa na Israel katika Bahari ya Mediterania ambapo ilitoa mkanda wa video ukionyesha maeneo zilikokuwa meli hizo na hivyo kutuma ujumbe kuwa inafuatilia nyendo zake kwa karibu.

Indhari hiyo ambayo ilikuwa na lengo la kuzuia Israeli kuingilia jiografia ya Lebanon, ilikuwa na thari kubwa katika azma ya Marekani ya kutaka kutatua mvutano huo wa mpaka kati ya Tel Aviv na Beirut. Aidha hatua hiyo ya Hizbullah ya kuonyesha mkanda huo wa video iliupelekea utawala wa Israel kurudi nyuma katika njama zake hizo za uvamizi. Sasa, kama Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon, alivyosema, rasimu ya mwisho iliyopokelewa kutoka upande wa Marekani kuhusu uwekaji mipaka ya bahari inaonekana kuwa chanya.

Michel Aoun, rais wa Lebanon kabla ya mazungumzo na mjumbe huyo wa Marekani alisema kuwa, nchi yake inafuatilia makubaliano yatakayolinda haki na utajiri wa Lebanon na kwamba mara baada ya mazungumzo hayo kumalizika kutakuwa na fursa ya kufufua uchumi wa nchi.

Mafuta na gesi ni muhimu kimkakati kwa uchumi wa sasa wa Lebanon, ambayo inakabiliwa na hali mbaya zaidi ya kiuchumi katika miongo ya hivi karibuni. Kiasi cha akiba ya gesi katika uwanja wa Karish inakadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni 1.3.

Seyed Hassan Nasrallah

Bila shaka pande husika zikifikia mapatano kuhusu uwekaji mipaka ya baharini, hatua ya kwanza ya mapatano hayo itaonyesha uwezo mkubwa wa Hizbullah wa kumzuia adui. Aidha mapatano hayo yanaashiria misimamo madhubuti ya Sayyed Hassan Nasrallah mlabala wa malengo ya uvamizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kuhusiana na hilo, Seyyed Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah, katika hotuba yake hivi karibuni, akizungumzia kupokelewa kwa pendekezo la maandishi la mpatanishi wa Marekani kuhusu kuwekewa mipaka ya baharini, ameiambia serikali ya Lebanon kwamba: "Ikiwa kesi ya kuweka mipaka itafikia mwisho wake unaotarajiwa, hayo yatakuwa ni matokeo ya umoja, ushirikiano na mshikamano wa kitaifa, na kwa msingi huo upeo wenye mwanga utafunguliwa mbele ya taifa la Lebanon."

 

Tags