Oct 04, 2022 10:55 UTC
  • Sheikh Isa Qassem: Utawala wa Aal Khalifa unataka kuwafanya Wabahrain watumwa

Ayatullah Sheikh Isa Qassem, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu Bahrain amesema, utawala wa kifalme wa Aal Khalifa unataka kuwafanya watu wa nchi hiyo watumwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Al Ahd, Ayatullah Sheikh Isa Qassem, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Bahrain, ameandika katika ukurasa wake wa Twitter: utawala wa Al-Khalifa unamfungia mlango kila mpiga kura na mwakilishi anayepigania uhuru na kujaribu kuwatia watu shingoni nira za utumwa.
Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Bahrain ameongeza kuwa, serikali inamuelekeza kwa makusudi na kwa nguvu kwenye utumwa kila raia na mwakilishi.
Hapo kabla pia, Sheikh Isa Qassem alieleza kwamba, kushiriki katika uchaguzi ulioitishwa hakufai na wala hakukubaliki kiakili, kidini na kwa mwenendo wa kimantiki; na akasema, hivi sasa hatua zinazochukuliwa zinalenga kuufanya uchaguzi usiwe na maana kwa kuonekana kitu kisicho na faida na maana kwa wananchi na kuugeuza kuwa wenzo kwa ajili ya mamlaka ya mtu binafsi.
Mfalme wa Bahrain Hamad bin Isa Aal Khalifa

Uchaguzi wa bunge nchini Bahrain umepangwa kufanyika mwezi ujao wa Novemba.

Tangu Februari 14, 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya wananchi dhidi ya utawala wa kifalme wa aila ya Aal Khalifa. Wabahrain wanataka kuwepo uhuru, itendeke haki na uadilifu, kuondolewe ubaguzi na kuwepo mfumo wa utawala uliochaguliwa na wananchi wenyewe.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakiulaani mara kwa utawala wa kifalme wa Aal Khalifa kwa kuwakandamiza wapinzani na kutaka yafanyike mageuzi katika mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo.../