Oct 04, 2022 11:31 UTC
  • Jumblatt na Netanyahu: Israel imesalimu amri kwa Hizbullah ya Lebanon

Kiongozi wa Chama cha Maendeleo cha Kisoshalisti cha Wadruzi wa Lebanon amesema, utawala wa Kizayuni wa Israel umesalimu amri kwa nguvu za Hizbullah katika kadhia ya uchoraji mipaka ya baharini.

Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha televisheni cha LBC, Walid Jumblatt ameeleza kuwa: Lebanon inahitaji nguvu za Hizbullah katika uwanja wa ulinzi.
Jumblatt amesisitiza kuwa, kwa kuzingatia tajriba ya uchoraji mipaka ya baharini, Hizbullah imefanya kazi ya diplomasia kwa umahiri.
Tangu mwanzoni mwa mwezi Julai na kufuatia kuingia meli ya kuchimba na kuhifadhi gesi iliyokodiwa na baraza la mawaziri la utawala haramu wa Israel karibu na eneo la baharini lenye gesi la Karish, Marekani imeshadidisha hatua za usuluhishi katika kadhia ya uainishaji mpaka wa baharini kati ya Lebanon na utawala wa Kizayuni.
Walid Jumblatt

Hayo yamejiri katika hali ambayo, harakati ya Hizbullah ya Lebanon imepinga vikali msimamo wa utawala ghasibu wa Kizayuni wa kutaka kujivutia maslahi zaidi katika suala hilo na imetahadharisha na kutoa indhari kwa njia tofauti kwamba kabla ya kuainishwa mpaka wa baharini wa Lebanon na wa eneo la kiuchumi la nchi hiyo katika Bahari ya Mediterania na kujulikana hatima ya maeneo ya gesi hususan ya Qana na Karish, ikatakabiliana na hatua yoyote ya kuvamia eneo la bahari na kufanya uchunguzi na uchimbaji gesi.

Wakati huohuo, Benjamin Netanyahu, kiongozi wa chama cha Likud na waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel, naye pia ameiambia Chaneli ya 14 ya televisheni ya utawala huo kuwa, makubaliano ya kuchora mipaka ya bahari ni makubaliano ya kuaibisha kwa utawala huo.
Netanyahu amedai kuwa, kwa muda wa miaka kumi, yeye hakuwa tayari kamwe kusalimu amri kwa Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, lakini waziri mkuu wa sasa wa Israel Yair Lapid, amesalimu amri kwa Nasrullah ndani ya miezi mitatu tu kwa sababu ametishwa na Nasrallah na atatoa rasilimali nyingi za gesi kwa Lebanon.../

Tags