Oct 05, 2022 03:02 UTC
  • Hamas: Kucheza muziki ndani ya Msikiti wa Nabii Ibrahim ni uchochezi dhidi ya Waislamu

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetangaza kuwa, sherehe ya kucheza ngoma na muziki ya walowezi wa Kizayuni ndani ya Msikiti wa Nabii Ibrahim mjini al Khalil (Hebron) ni jinai ya Kizayuni na kitendo hatari kinachochochea moja kwa moja hisia za Waislamu.

Ni baada ya walowezi wa Kizayuni kuandaa sherehe ya muziki na kucheza ngoma katika Msikiti wa Nabii Ibrahim ulioko mjini al Khalil siku ya Jumatatu iliyopita.

Harun Nasser El-Din mkuu wa ofisi ya Hamas huko Quds amesema kwamba hatua hiyo ya walowezi ni mwendelezo wa siasa za makusudi na zenye kuzusha mivutano za Wazayuni, ambazo zinalenga kudhibiti maeneo matakatifu.

Afisa huyo wa Hamas amezitaja juhudi za Wazayuni kuwa zitafeli na kwamba haziweza kufuta athari na alama za maeneo matakatifu wala kubadilisha ukweli wa historia.

Msikiti wa Nabii Ibrahim, al Khalil

Nasser El-Din amesema kuwa, wananchi wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan watatoa jibu mwafaka kwa vitendo hivyo na kutetea ardhi na maeneo yao matakatifu, na wataendelea na operesheni zao za kishujaa kwa njia yoyote inayowezekana.

Mwanachama huyo wa ngazi za juu wa Hamas amesisitiza ulazima wa kuweko mshikamano wa Wapalestina katika kuutetea Msikiti wa Al-Aqsa na kukabiliana na wavamizi na walowezi wa Kizayuni.

Hapo awali, Fawzi Barhoum, Msemaji wa harakati ya Hamas alitangaza kuwa, kupigwa marufuku ibada ya Swala katika Msikiti wa Nabii Ibrahim ni muendelezo wa uhalifu wa kupangwa dhidi ya taifa la Palestina na matukufu yake, na kwamba kimya cha kimataifa na hima ya baadhi ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni vimeupa utawala huo kiburi cha kutekeleza vitendo hivyo viovu.

Itakumbukwa kuwa, mwaka 2017 Kamati ya Urithi wa Dunia ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ilitangaza kwamba Msikiti wa Nabii Ibrahim huko al Khalil (Hebron) ni eneo la kihistoria linalomilikiwa na Wapalestina.