Oct 07, 2022 02:34 UTC
  • Yemen: Hakutakuwa na usitishaji vita hadi haki za watu wa Yemen zipatikane

Waziri Mkuu wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen ameutaja muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia na Umoja wa Mataifa kuwa zinahusika katika kufeli kwa usitishaji vita huko Yemen.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatano wiki hii lilitoa taarifa na kudai kuwa matakwa yaliyokithiri ya  Sana'a katika mazungumzo yanavuruga jitihada za umoja huo kwa ajili ya kufikia mapatano ya usitishaji vita. 

Tim Lenderking, Mjumbe Maalumu wa Marekani katika masuala ya Yemen pia ameitaka Sana'a ilegeze misimamo kuhusu suala la kurefusha muda wa mapatano ya kusitisha vita huko Yemen. 

Yemen na kufeli usitishaji vita 

Abdulaziz bin Habtoor Waziri Mkuu wa Serikali ya Uokovu wa Kitaifa ya Yemen  amejibu taarifa ya upendeleo ya Baraza la Usalama inayoituhumu Sana'a kuwa haijakuwa na mchango wowote muhimu katika kufanikisha usitishaji wa vita kwa kusema: Taarifa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa si ya kuwajibika na haikubaliki. Ameongeza kuwa, taarifa hiyo imeakisi mtazamo wa muungano wavamizi wa Yemen. 

Bin Habtoor amesema: "Ikiwa  takwa la kulipwa mishahara ya wafanyakazi na kuondolewa  mzingiro katika uwanja wa ndege wa Sana'a na bandari ya al Hudaydah ni msimamo mkali kwa maoni ya Baraza la Usalama, basi dunia nzima inapasa kufahamu kuwa sisi ni watu wenye msimamo mkali katika kupigania haki za wananchi wetu."

Bin Habtoor amesisitiza kuwa, nchi wanachama wa muungano vamizi wa Saudia huko Yemen, udhaifu wa Umoja wa Mataifa, Mjumbe Maalumu wa umoja huo katika masuala ya Yemen na unafiki wa jamii ya kimataifa ndivyo vinavyosababisha kufeli usitishaji vita huko Yemen.

Waziri Mkuu wa Serikali ya Uokoaji wa Kitaifa ya Yemen amesema: Haki na maslahi ya watu wa Yemen hayawezi kujadiliwa au kufumbiwa macho na makubaliano ya kusitisha vita hayawezi kufikiwa hadi haki za taifa letu zipatikane.

Tags