Oct 07, 2022 11:42 UTC
  • Hizbullah: Tutatumia nguvu za kijeshi ikiwa Israel itachimba mafuta na gesi kabla ya kufikiwa mwafaka

Mwakilishi wa Hizbullah katika Bunge la Lebanon amesema, harakati hiyo ya muqawama itatumia nguvu za kijeshi iwapo utawala haramu wa Kizayuni wa Israel utaamua kuchimba mafuta na gesi kabla ya kufikia makubaliano na Lebanon juu ya maeneo ya mpaka wa baharini zinayozozania.

Kuanzia Oktoba 2020, yalianza mazungumzo ya kiufundi kati ya utawala wa Kizayuni na Lebanon kwa usuluhishi wa Marekani ili kutatua mzozo uliopo kuhusiana na mipaka ya baharini ya pande mbili.
Tarehe 29 Septemba, balozi wa Marekani mjini Beirut Dorothy Shea alikutana na Rais Michel Aoun wa Lebanon katika Ikulu ya Baabda na kuwasilisha pendekezo la nchi yake kwa ajili ya kusuluhisha mzozo uliopo wa mpaka kwenye eneo la bahari kati ya Beirut na Tel Aviv.
Kwa mujibu wa tovuti ya habari ya Al-Arabi Al-Jadeed, Hussein Jashi, mbunge wa mrengo wa Hizbullah katika bunge la Lebanon ametangaza kuwa, iwapo Lebanon na utawala wa Kizayuni hazitofikia mapatano ya kuchora mipaka ya baharini, Israel haitakuwa na uwezo wa kuchimba mafuta na gesi katika kitalu cha Karish.
Mbunge huyo wa Hizbullah amebainisha kuwa Lebanon si nchi dhaifu kwa Israel kutaka kuitumia vibaya na kuchimba mafuta na gesi katika maeneo yanayozozaniwa kabla ya kufikiwa mwafaka; na akafafanua kwamba Lebanon, jeshi lake, watu wake na muqawama wao hawana mzaha hata chembe; na japokuwa hawataki vita, lakini hawatafumbia macho haki zao.

Jashi amesisitiza kuwa, anga inayotawala mazungumzo katika yasiyo ya ana kwa ana kati ya pande hizo mbili ni chanya na si hasha upinzani unaoonyeshwa na utawala wa Kizayuni ukawa ni wa kiujanja kwa sababu utawala huo hauna chaguo jengine isipokuwa kukubali mwafaka.

Wakati huohuo gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post limeripoti kuwa, waziri wa vita wa utawala haramu wa Israel Benny Gantz ameviamuru vikosi vya jeshi kujiweka katika hali kamili ya tahadhari karibu na mpaka na Lebanon kufuatia ripoti kwamba utawala huo ghasibu umeyakataa marekebisho ambayo Lebanon imetaka ifanyiwe hati ya mapatano yaliyopendekezwa na Marekani.../

Tags