Dec 01, 2020 02:35 UTC
  • Maandamano makubwa ya kupinga vitendo vya polisi vya utumiaji mabavu na ubaguzi nchini Ufaransa

Kufuatia kuongezeka migogoro ya kijamii na kisiasa nchini Ufaransa katika miezi ya hivi karibuni, kumeshuhudiwa ongezeko la vitendo vya polisi vya utumiiaji mabavu na ubaguzi wa rangi. Maovu hayo ya polisi ya Ufaransa yamepelekea kuibuka maandamano makubwa ya wananchi wanaolalamikia hali hiyo.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa, siku ya Jumamosi kulifanyika maandamano makubwa yaliyohudhuriwa na takribani watu 133,000. Idadi hiyo imepingwa na walioandaa maandamano hayo ambao wanasema watu zaidi ya nusu milioni walishiriki katika maandamano hayo yaliyofanyika katika miji  zaidi ya 70 kote Ufaransa kupinga polisi wanavyotekeleza ubaguzi wa rangi na kutumia mabavu dhidi ya wananchi.

Katika miezi ya hivi karibuni Ufaransa imeshuhudia maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi, ubepari na kulalamikia chuki dhidi ya Uislamu. Katika kujaribu kukandamiza maandamano hayo ya amani polisi nchini humo wamekuwa wakitumia mabavu na nguvu ziada. Hii ni katika hali ambayo wakuu wa Ufaransa wamekuwa wakidai kuwa nchi yao inaheshimu haki za binadamu, uhuru wa mtu binafsi na wa kijamii.

Christian Jacob, kiongozi wa chama cha Warepublican amepinga  kuwepo utumiaji mabavu katika idara ya polisi ya Ufaransa.

Pamoja na hayo, hivi karibuni klipu ya video imeenea katika mitandao ya kijamii ambamo polisi wa Ufaransa wameonekana wakimpiga vibaya kijana mwenye asili ya Afrika jambo ambalo limewakasirisha sana Wafaransa.

Klipu hiyo inaonyesha polisi wakimpiga kinyama mtu mwenye asili ya Afrika aliyetambuliwa kwa jina la Michel Zecler kwa sababu tu hakuwa amevaa barakoa!

Ukatili wa polisi Ufaransa

Baada ya klipu hiyo kusambazwa, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameandika katika ukurasa wake wa Facebook kuwa: "Taswira ya kuhujumiwa Michel Zecler haikubaliki na ni aibu kwa Wafaransa wote." Ameitaka serikali ichukue hatau za haraka za kurejesha imani ya wananchi kwa polisi.

Hayo yanajiri wakati ambao wiki iliyopita serikali ya Macron ilipendekeza muswada wa sheria wa kuzuia watu kuwapiga picha polisi. Muswada huo ulilalamikiwa vikali na watetezi wa haki za binadamu na waandishi habari. Wakosoaji wanasema endapo muswada huo utapitishwa na kuwa sheria, basi itakuwa rahisi kuficha jinai zinazotendwa na polisi.

Hali kadhalika katika wiki za hivi karibuni polisi nchini Ufaransa wamelaumiwa kwa kutumia mabavu kuzima maandamano ya watu wanaolalamikia sera za serikali za chuki dhidi ya Uislamu. Vitendo hivyo vya mabavu vya polisi na jairbio la serikali kuzuia upigaji picha polisi wanapotenda jinai ni mambo ambayo yanabainisha wazi kuwa nara za uhuru katika nchi hiyo ya Ulaya ni hadaa tupu.

Macron

Yusuf Ozhan mtaalamu wa masuala ya kisiasa ameandika makala yenye anwani inayosema: "Chuki dhidi ya Uislamu Ufaransa sasa imebadilika kuwa sera ya daima". Katika makala hiyo ameandika: "Wakuu wa Ufaransa wanatumia kisingizio cha kulinda usekulari kueneza ubaguzi dhidi ya Waislamu na sasa vitendo hivyo vyao vimepata kinga ya kisheria."

Inaelekea kuwa, wakuu wa Ufaransa wanatumia nara ya uhuru kutetekea ukatili wa polisi nchini humo lakini Wafaransa waliowengi wamechoshwa na sera hiyo na sasa wamejitokeza mitaani kubainisha upinzani wao.

 

Tags