Jul 07, 2018 02:42 UTC
  • Joto kali laua makumi ya watu mashariki mwa Canada

Wimbi la joto kali ambalo halijawahi kushuhudiwa limesababisha vifo vya watu 33 katika mkoa wa Quebec mashariki mwa Canada.

Duru za habari zimearifu kuwa, watu 18 miongoni mwao wamepoteza maisha katika mji wa Montreal, unaoshuhudia joto kali lenye kupindukia nyuzijoto 37, lakini kutokana na ukavu wa joto lenyewe, kiwango cha joto hilo kinahisika kupindikia nyuzijoto 47.

Waziri Mkuu, Justin Trudeau ametuma salamu za rambirambi kwa familia, jamaa na marafiki wa wahanga wa janga hilo la kimaumbile. Amendika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa: Fikra zangu ziko pamoja na wapendwa wa watu walioaga dunia kutokana na joto kali mkoani Quebec.

Kijana mkoani Quebec akijaribu kupunguza makali ya joto

David Kaiser, afisa wa Idara ya Afya ya Umma amesema aghalabu ya walioga dunia katika mkasa huo ni wanaume wenye umri wa kati ya miaka 53 na 85 haswa wanaoshi peke yao katika majumba ya kibinafsi bila viyoyozi. Amesema wazee na watu wenye matatizo ya akili wapo katika hatari kubwa ya kupoteza maisha katika kipindi hiki cha joto kali.

Bara Ulaya, Amerika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati ni katika maeneo yanayoshuhudia wimbi la joto kali wakati huu. Mwezi Mei mwaka huu, watu zaidi ya 65 waliripotiwa kupoteza maisha kutokana na joto kali katika mji mkuu wa Pakistan, Karachi.

 

Tags