Jan 13, 2019 07:44 UTC
  • Utafiti: Uchafuzi wa hali ya hewa duniani umekithirisha kuharibika kwa mimba

Utafiti mpya umebainisha kuwa, uchafuzi wa hali ya hewa duniani umepelekea kuongezeka idadi ya mimba kuharibika au wanawake kujifungua kabla ya wakati.

Dakta Matthew Fuller wa Chuo Kikuu cha Utah mjini Salt Lake nchini Marekani aliyeongoza utafiti huo amesema kuwa, gesi hatari ya 'nitrogen dioxide' inayotokana na fueli haswa dizeli inaongeza uwezekano wa mimba kuharibika au mwanamke kujifungua kabla ya wakati kwa asilimia 16.

Amesema kwa mujibu wa utafiti wao, athari ya hali chafu ya hewa kwa mimba changa ya kuanzia mwezi mmoja hadi mitatu ni sawa na athari ya tumbaku kwa mimba ile.

Ripoti ya utafiti huo iliyochapishwa katika jarida la Fertility and Sterility inaonesha kuwa, aghalabu ya wanawake 1,300 ambao mimba zao ziliharibika kati ya mwaka 2007 na 2015 katika mji wa Salt Lake, waliathirika kutokana na kuvuta hewa chafu.

Mbali na Marekani, uchafuzi mkubwa wa hewa unashuhudiwa katika nchi za India na China

Juni mwaka jana, Umoja wa Mataifa ulitahadharisha kuhusu ongezeko la uchafuzi wa hali ya hewa na taathira zake kwa viumbe kote duniani, ambapo Marekani ilitajwa kuwa ya kwanza kati ya nchi zilizoendelea kiviwanda kwa kuchafua mazingira na hali ya hewa.

Pamoja na hayo Rais Donald Trump wa Marekani aliiondoa nchi hiyo katika Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Paris licha ya malalamiko makubwa ya jamii ya kimataifa.   

Tags