Apr 08, 2019 07:57 UTC
  • Uturuki yakosoa matamshi ya kijuba ya Waziri Mkuu wa Israel

Uturuki imekosoa vikali matamshi wa Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu aliyedai kuwa iwapo ataibuka mshindi katika uchaguzi mkuu ujao, basi atauunganisha rasmi Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na maeneo mengine ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu, chini ya mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne".

Mevlut Cavusoglu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kuwa, "Ukingo wa Magharibi ni eneo la Wapalestina linalokaliwa kwa mabavu na Israel, kwa kukiuka sheria za kimataifa."

Amesema matamshi ya kijuba ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwa ajili kwa kuwaraia wapiga kura katu hayawezi kubadilisha ukweli huo.

Naye Ibrahim Kalin, msemaji wa Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema kauli hiyo iliyotolewa na Netanyahu siku ya Jumamosi kuelekea uchaguzi wa Jumanne, ni mfano mwingine wa Netanyahu kutumia kauli za kisiasa kuhalalisha ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Wapalestina.

Vitongoji vya walowezi wa Kizayuni Ukingo wa Magharibi

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu Palestina HAMAS imesema kuwa lengo la mpango wa Marekani unaoitwa 'Muamala wa Karne' ni kuutenganisha Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Julai mwaka jana, Bunge la utawala ghasibu wa Israel (Knesset) lilipasisha sheria ambayo inazipokonya mamlaka ya kisheria na kushughulikia kesi Mahakama za kieneo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuhamishia kesi hizo katika mahakama inayojulikana kama Mahakama Kuu, kwa maana kwamba Mpalestina atakayetaka kuwashtaki Wazayuni atalazimika kuwasilisha mashtaka yake katika mahakama za Waisrael.

Tags

Maoni