Apr 12, 2019 14:57 UTC
  • Upinzani: Uingereza haipaswi kumkabidhi Julian Asange kwa Marekani

Kiongozi wa chama Leba nchini Uingereza amekosoa vikali kitendo cha kutiwa mbaroni mjini London mwasisi wa mtandao unaojishughulisha na kufichua siri na kashfa wa WikiLeaks, Julian Assange.

Jeremy Corbyn ambaye ni kinara wa kambi ya upinzani bungeni nchini Uingereza amesema serikali ya London inapaswa kuzuia jitihada zozote za kusafirishwa nchini Marekani Julian Assange.

Wakili wa Assange, Jen Robinson amesema kuwa, mteja wake amekamatwa kutokana na ombi la Marekani ambayo inataka apelekwe nchini humo kwa ajili ya kufunguliwa mashitaka ya kuvujisha nyaraka za serikali.

Kitendo hicho cha kukamatwa mwandishi huyo wa habari kimeendelea kukosolewa katika kona mbalimbali za dunia.

Maria Zakharova, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia ametoa ujumbe akisema kuwa: "Mkono wa demokrasia uko katika kukandamiza uhuru wa kujieleza."

 

Assange akikamatwa  na polisi ya UK

Maandamano yalishuhudiwa jana Alkhamisi nje ya ubalozi wa Ecuador mjini London baada ya polisi ya Uingereza kumtia mbaroni mwasisi huyo wa mtandao unaofichua fedheha nyingi za nchi na viongozi mbalimbali duniani wa WikiLeaks, Julian Assange, ambaye amekuwa akiishi ubalozini hapo tokea mwaka 2012.

Assange alianzisha mtandao huo wa kufichua siri mwaka 2006, na mwaka 2010  mtandao huo ukapata umashuhuri sana duniani kwa kusambaza video na picha za mauaji ya kutisha yaliyofanywa na askari wa Marekani nchini Iraq na Afghanistan iliyopewa jina 'Collateral Murder'.

 

Tags