Jul 01, 2019 01:31 UTC
  • Mazungumzo baina ya serikali na wapinzani nchini Venezuela kuanza karibuni hivi

Mazungumzo baina ya wawakilishi wa serikali na wapinzani nchini Venezuela yanatarajiwa kuanza hivi karibuni lengo likiwa ni kufanya juhudi za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo.

Duru za karibu na pande mbili zimetangaza kuwa, pamoja na kuwa, mahala pa kufanyika mazungumzo hayo bado hapajajulikana, lakini mazungumzo baina ya pande mbili yanatarajiwa kufanyika katika sikuu chache zijazo.

Hadi sasa serikali ya Venezuela na wapinzani wamekutana mara mbili huko Norway lakini duru mbili hizi za mazungumzo hazikupelekea pande mbili kufikia makubaliano.

Machafuko na ghasia nchini Venezuela zilishtadi baada ya Juan Guaidó kujitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo kuanzia mwezi Januari mwaka huu.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

Katika miezi ya karibuni Marekani na waitifaki wake wameendesha mashambulizi na vita vikubwa vya kipropaganda dhidi ya serikali ya Caracas sambamba na kuiwekea Venezuela vikwazo vikali na kulishinikiza jeshi na vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo kuacha kuiunga mkono serikali ya Rais Maduro, lakini njama zote hizo zimegonga mwamba. 

Aidha madola ya Magharibi yamekuwa yakitangaza wazi kumuunga mkono kiongozi huyo wa upinzani kwa lengo la kutaka kumuondoa madarakani Nicolás Maduro, rais halali wa nchi hiyo aliyechaguliwa na wananchi.

Mkabala na madola hayo ya Magharibi, nchi nyingi kama vile Russia, China, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Afrika Kusini zimetangaza kumuunga mkono rais anayetambuliwa kikatiba, yaani Nicolás Maduro.

Tags