Jul 06, 2019 08:16 UTC
  • Rais wa Venezuela asisitiza kuunga mkono mazungumzo na wapinzani

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela amesisitiza kuwa, serikali yake inaunga mkono na kuheshimu mchakato wa kuendelezwa mazungumzo na wapinzani wake kwa usimamizi wa Norway.

Rais Maduro amesema kupitia ujumbe wake kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, serikali yake inaunga mkono kuweko mazungumzo ya daima yenye lengo la kuzipatia ufumbuzi hitilafu za kisiasa baina yake na wapinzani.

Hii si mara ya kwanza kwa Rais Nicolas Maduro kusisitiza kwamba, serikali yake ipo tayari kuendeleza mazungumzo na wapinzani.

Licha ya kuweko ukwamishaji mambo unaofanywa na wapinzani, lakini hadi sasa serikali ya Venezuela imekutana mara mbili na wapinzani katika mazungumzo huko Norway.

Hata hivyo hadi sasa mazungumzo hayo hayajaweza kuzaa matunda kutokana na sababu mbalimbali.

Juan Guaido, kiongozi wa upinzani nchini Venezuela

Wakati huo huo, imeelezwa kuwa, mazungumzo baina ya wawakilishi wa serikali na wapinzani nchini Venezuela yanatarajiwa kuanza hivi karibuni lengo likiwa ni kufanya juhudi za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo.

Machafuko na ghasia nchini Venezuela zilishtadi baada ya Juan Guaidó kujitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo kuanzia mwezi Januari mwaka huu.

Katika miezi ya karibuni Marekani na waitifaki wake wameendesha mashambulizi na vita vikubwa vya kipropaganda dhidi ya serikali ya Caracas sambamba na kuiwekea Venezuela vikwazo vikali na kulishinikiza jeshi na vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo kuacha kuiunga mkono serikali ya Rais Maduro, lakini njama zote hizo zimegonga mwamba. 

Tags