Jul 17, 2019 02:30 UTC
  • Sisitizo la wapinzani wa Venezuela la kuendelea kushiriki katika mazungumzo na serikali ya Caracas

Baada ya duru tatu za mazungumzo baina ya serikali ya Venezuela na wapinzani yenye lengo la kufikia utatuzi wa pamoja na kuikwamua nchi hiyo katika kinamasi cha mgogoro wa kisiasa, wapinzani wa nchi hiyo wamethibitisha kwamba, wataendelea kushiriki katika mazungumzo na wawakilishi wa serikali huko nchini Barbados katika Bahari ya Caribbean.

Licha ya kuwa imepita miezi mingi sasa tangu Venezuela ilipokumbwa na mgogoro wa kisiasa na machafuko ya ndani, lakini hatua ya Juan Guaido, kiongozi wa upinzani ya kujitangaza Januari mwaka huu kuwa, Rais wa nchi na hilo kuungwa mkono na Marekani na washirikika wake, iliufanya mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo kuingia katika hatua mpya. Miezi ya hivi karibuni imeshuuhudia ndani ya Venezuela wapinzani wakichukua hatua za kutaka kuiondoa madarakani serikali halali ya Rais Nicolas Maduro. Aidha kwa upande wa nje, walimwengu walishuhudia kushadidi siasa za chuki za Marekani na waitifaki wake dhidi ya Venezuela.

Licha ya hayo yote, lakkini njama za wapinzani ndani ya Venezuela  kwa uungaji mkono wa Marekani pamoja na mashinikizo ya kiuchumi ya Washington hazijaweza kuiondoa madarakani serikali ya Rais Nicolas Maduro.  Ukweli wa mambo ni kuwa, kutokuwa na nafasi ya kuzingatiwa Juan Guaido kiongozi wa upinzani kwa upande mmoja na himaya na uungaji mkono mkubwa wa wananchi wa Venezuerla kwa Rais Maduro kwa upande wa pili sambamba na ghadhabu za wananchi hao kwa uingiliaji wa Washington katika masuala ya ndani ya nchi yao ni mambo ambayo yamesambaratisha njama zote za ndani na za nje za kutaka kumuondoa madarakani Rais Maduro.

Rais Nicolas Maduro wa Venezuela

Filihali kumeanza hatua na marhala mpya ya kutaka kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa Venezuela. Licha ya kuwa, huko nyuma, viongozi wa Caracas walitangaza mara chungu nzima juu ya nia yao ya kufanya mazungumzo yenye lengo la kuzitafutia ufumbuzi hitilafu zilizopo nchini humo, lakini  wapinzani waling'angia takwa lao la kuondoka madarakani Rais Maduro.

Kwa kuzingatia kushindwa wapinzani kufikia malengo yao kupitia njia ya mashinikizo, inaonekana kuwa, sambamba na kulegeza kamba kuhusiana na nara na siasa zao haribifu, sasa wamediriki kwamba, mazungumzo ndio njia bora na mwafaka ya kuyapatia ufumbuzi matatizo ya kisiasa ya nchi hiyo. Pamoja na hayo, viongozi wa Washington wangali wanafuatilia siasa za kutaka kuvuruga mazungumzo hayo.

Washington inafanya juhudi za kuwapa maagizo wapinzani na hivyo kufunga mlango wowote ule wa kupatiwa ufumbuuzi mgogoro wa Venezuela kwa njia ya amani na kwa muktadha huo kuandaa uwanja wa kuishambulia kijeshi nchi hiyo. Samuel Moncada balozi na mwakilishi wa kudumu wa Venezuela katika Umoja wa Mataifa anasema kuwa: 

Serikali ya Rais Donald Trump na washirika wake wanataka kukwamisha mazungumzo ya wapinzani na serikali ya Caracas ili mgogoro huo wa kisiasa uendelee kushuhudiwa katika nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Juan Guaido, kiongozi wa upinzani wa Venezuela anayeungwa mkono na Marekani

Viongozi wa Marekani wanataka mgogoro wa kisiasa wa Venezuela uendelee kushuhudiwa ili waimarishe upenyaji wao si katika nchi hiyo tu bali katika nchi za Amerika Latini kwa ujumla na kutumia fursa hiyo kustafidi na mafuta na vyanzo vya utajiri vya nchi za eneo hilo kama dhahabu, gesi, almasi na utajiri mwingine.

Hivi sasa imeamuliwa kuwa, mazungumzo baina ya wawakilishi wa serikali na wapinzani yataendelea kufanyika ili kutafuta njia za kufikia makubaliano. Licha ya kuwa, njama za Marekani nazo za kutaka kuwa na taathira kwa mwenendo wa mazungumzo hayo sambamba na kuyakwamisha zingali zinaendelea, lakini Rais Maduro ametangaza kuwa, ana matumaini na mwenendo wa mazungumzo hayo na kupatikana natija nzuri.

Jorge Arreaza, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Venezuela anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Licha ya mashinikizo yote ambayo Venezuela inaandamwa nayo, lakini mwisho wa siku ni amani ndiyo itakayoshinda katika nchi hiyo.

Tags