Jul 21, 2019 07:49 UTC
  • Kuendelea mazungumzo ya serikali ya Venezuela na wapinzani licha ya vitisho vya Wamagharibi

Mashinikizo na vitisho vya Marekani na nchi za Ulaya dhidi ya Venezuela, vimeongezeka huku mazungumzo ya kutafuta njia ya kuiodoa nchi hiyo kwenye mgogoro wa kisiasa yakiwa yanaendelea kati ya serikali na wapinzani.

Katika uwanja huo wawakilishi wa serikali ya Venezuela na wapinzani waliokutana nchini Barbados kwa ajili ya mazungumzo, wametangaza kufikia hatua chanya za kutatua mgogoro huo wa kisiasa. Mazungumzo kati ya serikali na wapinzani yanaendelea  nchini Barbados huku wengi wakitumai  kwamba yatafungua fundo la sasa la mgogoro wa Venezuela na hivyo kuziwezesha pande mbili kufikia njia ya kuhitimisha mkwamo wa kisiasa wa hivi sasa nchini humo. Kuhusiana na suala hilo, Jorge Rodríguez, Waziri wa Mawasiliano wa Venezuela na mkuu wa ujumbe uliotumwa na Rais Nicolás Maduro katika mazungumzo hayo amesema: “Tunaendelea na mazungumzo na tunatangaza kuheshimu kikamilifu misingi yake iliyoainishwa. Tunawataka wote kufanya juhudi za kuunga mkono jitihada hizi za mazungumzo baina ya Wavenezuela." Hii ni katika hali ambayo sambamba na kuongezeka kasi ya mwenendo wa mazungumzo hayo na kuonekana ridhaa ya pande mbili, vitisho na mashinikizo dhidi ya serikali ya Caracas, nayo yameongezeka.

Venezuela imesimama imara kukabiliana na Marekani

Katika miezi ya hivi karibuni viongozi wa Marekani wamefanya njama nyingi kupitia kuwaunga mkono wapinzani wa ndani wa nchi hiyo ya Amerika ya Latini, hususan Juan Guaidó, kiongozi wa wapinzani na pia kutekeleza siasa za vikwazo vikali katika sekta ya mafuta, gesi, nishati na benki ili kuzidisha mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya serikali ya Rais Nicolás Maduro. Hivi sasa pia viongozi wa White House wanakusudia kuzidisha mashinikizo kwa lengo la kuathiri mwenendo wa mazungumzo ya pande mbili hizo na kisha kuyafelisha kabisa mazungumzo hayo. Kwa mtazamo wa Marekani, kufikiwa utatuzi wa kuiondoa nchi hiyo kwenye mgogoro wa kisiasa katika mazungumzo ya sasa, ni sawa na kushindwa kikamilifu siasa za kigeni za Washington dhidi ya Venezuela. Katika hatua mpya ya serikali ya Rais Donald Trump dhidi ya Venezuela, Ijumaa iliyopita Wizara ya Fedha ya Marekani iliwawekea vikwazo maafisa wanne wa jeshi la Venezuela. Katika hatua nyingine, Shirika la Ustawi wa Kimataifa la Marekani (USAID) limetenga kiasi cha Dola milioni 40 kwa ajili ya wapinzani wa Venezuela. Hatua hizo za Washington zinatekelezwa katika hali ambayo Umoja wa Ulaya pia katika hatua inayokwenda sambamba na siasa za Marekani, umewatishia viongozi wa Venezuela kwamba iwapo mazungumzo yataendelea kutokuwa na natija kwa ajili ya kutatua mzozo wa kisiasa wa nchi hiyo, basi utaiwekea vikwazo vipya serikali ya Rais Nicolás Maduro sambamba na kuongeza majina mapya ya viongozi wa serikali kwenye orodha nyeusi ya vikwazo.

Federica Mogherini, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya

Katika uwanja huo Federica Mogherini, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya amesema: “Iwapo mazungumzo yanayoendelea hayatofikia natija muhimu, umoja huu utachukua hatua zaidi.” Maneno hayo yamekabiliwa na radiamali kali kutoka kwa serikali ya Caracas. Viongozi wa Venezuela, sambamba na kupinga msimamo huo wa Umoja wa Ulaya, wametangaza kwamba, umoja huo una lengo la kuzuia mazungumzo hayo yasitatue mzozo uliopo kwa njia ya amani. Kuhusiana na suala hilo Rais Nicolás Maduro amesema: “Federica Mogherini, Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya anataka  kutumia matamshi yake hayo kuibua mashinikizo zaidi kwenye mazungumzo kati ya serikali na wapinzani wa Venezuela, hata hivyo matamshi hayo ni ya aibu na yasiyo ya kimantiki.” Baada ya kufeli hujuma za kila upande za Marekani na washirika wake dhidi ya Venezuela, hivi sasa Washington na Umoja wa Ulaya zinajitahidi kupitia siasa za mashinikizo na vitisho, kushadidisha vikwazo na kuwaunga mkono kifedha wapinzani, ili zipate kuharibu mwenendo wa mazunguzo hayo ya serikali na wapinzani, kwa kuwa Washington inaamini kuwa baada ya kufeli mazungumzo hayo, itaweza kufanikisha siasa zake za uingiliaji na za kupenda vita huko Venezuela na katika eneo zima la Amerika ya Latini. Hata hivyo, licha ya ukwamishaji mambo huo wa kila upande, viongozi wa Venezuela ambao wana uungaji mkono wa wananchi wamekuwa wakisisitizia umuhimu wa kuendelezwa mazungumzo kwa ajili ya kufikiwa amani, kuishi pamoja kwa amani na kutatuliwa masuala yenye tofauti za kisiasa kwa msingi wa sheria.

Tags