Aug 03, 2019 07:39 UTC
  • Kujitoa Marekani katika mkataba wa INF; hatua mpya ya kuzidi kuvuruga uthabiti na amani ya dunia

Tangu Donald Trump alipoingia madarakani na kushika hatamu za urais wa Marekani, ameamua kufuata muelekeo wa kudharau na kujitoa kwenye mikataba ya kimataifa ikiwemo ya silaha.

Hatua iliyochukuliwa na Washington tarehe Pili Februari mwaka huu ya kusimamisha utekelezaji wa mkataba wa Silaha za Nyuklia za Masafa ya Kati (INF) iliupa ulimwengu changamoto kubwa, ambayo ni kulegalega mikataba iliyopo ya silaha na kuashiria kuibuka mashindano mapya ya uundaji silaha hatari. Marekani ilisisitiza wakati huo kwamba, endapo katika muda wa miezi sita, Russia itashindwa kutekeleza vipengele vya makataba huo, ifikapo Agosti Pili itajitoa rasmi kwenye INF.

Hatimaye jana Ijumaa ya tarehe Pili Agosti, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo alitangaza rasmi kujitoa nchi yake katika mkataba wa kupiga marufuku silaha za nyuklia za masafa ya kati, huku akiibebesha lawama Russia ya uvunjaji huo wa makubaliano uliofanywa na Washington.

Mkataba wa INF ulisainiwa na aliyekuwa Kiongozi wa Urusi ya zamani (USSR) Mikhail Gorbachev (kulia) na rais wa wakati huo wa Marekani Ronald Reagan (kushoto)

Katika ujumbe aliotuma kwenye ukurasa wake wa Twitter hapo jana, Pompeo alikariri madai kwamba Russia haiheshimu wala haitekelezi makubaliano ya INF na kuandika kuwa: "Tarehe Pili Februari 2019, Marekani ilitoa fursa ya miezi sita kwa Russia kurejea kwenye utekelezaji wa mkataba huu. Russia imepinga, kwa hivyo makubaliano haya yanafikia tamati leo. Marekani haitabaki kuwa sehemu ya makubaliano ambayo wengine wanayakiuka. Russia ndiyo inayobeba dhima kamili," alidai Pompeo.

Serikali ya Trump pamoja na shirika la kijeshi la NATO, zote zimeituhumu Russia kuwa imekiuka mktaba wa INF na kudai kwamba, nchi hiyo imeunda makombora ya Cruise yanayopaa umbali wa kilomita zaidi ya 500, yakiwa na uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia; madai ambayo Russia imeyakanusha.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetoa jibu kwa hatua hiyo ya Washington kupitia taarifa maalumu na kutangaza kuwa, utekelezaji wa mkataba unaopiga marufuku makombora ya nyuklia ya masafa ya kati umefikia tamati Ijumaa ya jana ya tarehe Pili Agosti, kutokana na hatua iliyochukuliwa na Marekani.

Mkataba wa INF uliwezesha kutokomezwa makombora ya masafa mafupi na ya masafa ya kati ya Cruise na ya balestiki  yanayokata masafa ya umbali wa kilomita 500 hadi elfu tano . Kwa kipindi cha miaka kadhaa iliyopita Washington na Moscow zimekuwa zikituhumiana kukiuka mkataba huo muhimu wa silaha. Wakati Marekani iliposimamisha utekelezaji wa mkataba wa INF Februari Pili mwaka huu, ilitoa sharti pia kwamba, itaendelea kubaki kwenye makubaliano hayo kama Russia nayo itayaheshimu na kuyatekeleza; na ikatoa muhula wa miezi sita kwa Moscow kufanya hivyo. Siku chache baada ya uamuzi huo wa Marekani, Russia nayo ikachukua hatua ya kujibu mapigo, ambapo mbali na kutaja masuala kadhaa likiwemo la uwekwaji mfumo wa kutungulia makombora wa Marekani mashariki ya Ulaya, kwa amri ya rais wa nchi hiyo Vladimir Putin, nayo pia ikatangaza kusitisha utekelezaji wa mkataba huo wa INF.

Kuvunjwa mkataba wa kupiga marufuku silaha za nyuklia za masafa ya kati kumezusha wasiwasi mkubwa kwa nchi za Ulaya, kwani nchi hizo sasa zitashuhudia kwa mara nyingine mashindano ya uundaji silaha kati ya Washington na Moscow katika bara hilo. Lengo la serikali ya Trump ni kuitumbukiza Russia kwenye mtego wa mashindano mapya ya uundaji silaha kwa madhumuini ya kudhoofisha uwezo wake wa kiuchumi. Suala hilo alisisitizia pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov mnamo tarehe 13 Aprili mwaka huu alipohutubia Baraza la Sera za Nje na Ulinzi la Russia. Lavrov alisema: Wanaopendelea mashindano ya uundaji silaha wamekuwa na sauti ya juu katika serikali ya Washington, hata hivyo Russia haitajiingiza kwenye mashindano ya uundaji silaha. 

Kufuatia kujitoa Marekani na Russia katika mkataba wa INF, mnamo wiki zijazo, Washington itaanza kuyafanyia majaribio makombora ya aina hiyo. Shirika la habari la Reuters limewanukuu maafisa kadhaa waandamizi wa serikali ya Marekani ambao hawakutaka kutajwa majina yao na kuripoti kwamba, kuanzia sasa na kuendelea, Washington haitajifunga tena na kutounda au kutorundika makombora ya masafa ya kati yenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia.

Ukweli ni kwamba kuendelea mwenendo ulioanzishwa na Marekani wa kujitoa kwenye mikataba ya kimataifa ya udhibiti wa silaha, kutazidi kuvuruga amani na uthabiti katika uga wa kimataifa. Kuvunjwa mkataba wa INF kunamaanisha kushtadi na kupanuka wigo wa makabiliano ya kimakombora na kinyuklia kati ya Marekani na Russia, na kuyaingiza madola mengine ya nyuklia kama China kwenye makabiliano hayo. Hali hiyo itasababisha kutokea mtibuko wa amani na uthabiti ambao haujawahi kushuhudiwa katika Zama za Baada ya Vita Baridi (Post-Cold War era). Kuendelea kwa mwenendo huu si tu kutashamirisha uundaji silaha zilizopigwa marufuku kulingana na mkataba wa INF na hivyo kujitokeza mashindano mapya ya uundaji silaha katika uga wa kimataifa, lakini pia kutahatarisha sana amani na uthabiti wa dunia nzima.../

Tags

Maoni