Sep 11, 2019 02:31 UTC
  • Ukosoaji wa Russia kwa nafasi haribifu ya Magharibi katika Ghuba ya Uajemi

Baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza kuiondoa nchi hiyo katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia mashuhuri kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) mnamo tarehe 8 Mei mwaka uliopita, alianza kutekeleza mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa dhidi ya Iran.

Moja ya iliyokuwa mipango muhimu ya Marekani katika uwanja huo ni kufikisha mauzo ya mafuta ya Iran kwenye kiwango cha sifuri. Vikwazo vya kiuchumi ambavyo havijawahi kushuhudiwa pamoja na mashinikizo hayo ya Washington yamepelekea kushadidi mzozo baina yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo moja ya mivutano hiyo ni katika Lango Bahari la Hormoz na Ghuba ya Uajemi.

Hatua ya Marekani ya kuongeza pakubwa uwepo wake wa kijeshi na kuanzisha muungano wa kimataifa wa baharini ambao hadi sasa haujawa na wanachama ghairi ya watatu tu, ililenga eti kudhamini usalama wa meli katika eneo la Ghuba ya Uajemi. Marekani imepata pigo katika hilo, kwani hata madola ya Ulaya ukiitoa Uingereza yamekataa kujiunga na muungano huo.

Hatua haribifu na hatarishi kwa usalama za Marekani na washirika wake hususan Uingereza katika ukanda wa Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Hormoz, imekosolewa vikali na Russia. Kuhusiana na hilo, Sergey Shoygu, Waziri wa Ulinzi wa Russia, Jumatatu ya juzi Septemba 9 alisisitiza baada ya kikao cha pamoja cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni na wa Ulinzi wa Russia na Ufaransa (2+2) kwamba, endapo meli za mafuta za zinazokwenda katika maeneo mbalimbali duniani hazitatuhumiwa kwamba, zinakiuka sheria za kimataifa, basi hali ya mambo katika eneo la Ghuba ya Uajemi itakuwa tulivu na salama.

Waziri wa Ulinzi wa Russia amesema dhahir shahir kwamba: Kwa mujibu wa tathmini yetu ni kuwa, madhali madola ya Magharibi yanakwamisha mambo katika mazingira ya kisiasa na yanaleta usumbufu kwa meli za Iran, basi hali ya kulegalega na isiyo tulivu itaendelea kushuhudiwa. Hali ya mambo katika Ghuba ya Uajemi itabakia katika anga ya kawaida, pale tu uingiliaji mambo utakapokomeshwa na wakati huo huo kusitishwa hatua za kuzikamata meli za Iran katika maeneo mbalimbali ya dunia kwa kisingizio eti cha kukiuka sheria za kimataifa. Ni katika mazingira haya tu, ndipo Ghuba ya Uajemi itaikoka na aina yoyote ile ya mivutano na mizozo, na kwa mintarafu hiyo hakutakuwa na haja ya kuchukuliwa hatua mpya za kuleta uthabiti katika eneo hilo.

Matamshi hayo ya afisa wa ngazi za juu wa kijeshi wa Russia yanazionyeshea kidole cha lawama hatua haribifu na za kuzusha mivutano za Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi ambazo znafanyika katika fremu ya malengo jumla ya kufikisha mauzo ya mafuta ya Iran kwenye kiwango cha sifuri na si tu kuiwekea vikwazo kikamilifu vya mafuta Iran na kuwatisha wanunuzi wa mafuta ya taifa hili, bali hizi ni njama zenye wigo mpana za kuzishikilia meli za mafuta za Iran katika maeneo mbalimbali ya dunia.

Mfano hai katika uwanja huo ni kadhia ya meli ya mafuta ya Adrian Darya ambayo hapo kabla ilikuwa na jina la Grace 1 na ambayo ilishikiliwa na kuzuia na kikosi maalumu cha Uingereza katika Lango Bahari la Jabal al-Tariq kwa kisingizio eti cha kukiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Syria. Hatimaye baada ya siku 40, Agosti 15 mwezi uliopita, Uingereza ililazimika kuiachilia meli hiyo. Hata hivyo, serikali ya Marekani iliendelea kuifuatilia meli hiyo iliyokuwa ikielekea mashariki mwa Mediterenia hata baada ya kubalishwa jina na umiliki wake.  Si hayo tu, Marekani ilitishia kuziwekea vikwazo nchi kama Ugiriki, Uturuki na Lebanon ambazo kulikuwa na uwezekano wa meli hiyo kutia nanga huko endapo zingeipatia huduma meli hiyo.

RaisDonald Trump wa Marekani akiteta jambo na Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia

Marekani ilijaribu hata kumnunua nahodha wa meli hiyo kwa kitita kikubwa cha fedha ili atekeleze matakwa ya Washington, lakini ikafeli pia katika hilo. Ripoti zinaonyesha kuwa, Brian Hook, mwakilishi maalumu wa Washington katika masuala ya Iran alimtumia ujumbe Akhilesh Kumar, nahodha wa meli ya Adrian Dariya mwenye asili ya India na kumpendekezea kitita kikubwa cha fedha ili aipelekea meli hiyo sehemu mwafaka ambayo itawezekna kuikamata meli hiyo. Hata hivyo, nahodha huyo jasiri alikataa rushwa hiyo na kupelekea awekewe vikwazo na Wizara ya Hazina ya Marekani.

Utendaji huu wa Marekani si tu kwamba, unakiuka sheria za kimataifa, bali umekuwa sababu ya kuibuka hali isiyoaminika na hatarishi kwa usalama wa meli katika Ghuba ya Uajemi na Lango Bahari la Horzom. Kwa kuzingatia hilo, serikali ya Moscow inayataka madola ya Magharibi hususan Marekani yabadilishe na kurekebisha muamala, mwenendo na utendaji wao hu hasi kwa Iran, ili kwa njia hiyo kuandaliwe uwanja na mazingira ya kupatikana amani na uthabiti katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Tags

Maoni