Sep 11, 2019 03:23 UTC
  • Tetemeko ndani ya kambi ya Trump, Bolton atimuliwa serikalini

Rais wa Marekani, Donald Trump amemtimua serikalini, mshauri wa usalama wa taifa wa White House, John Robert Bolton.

Hatua hiyo ilitangazwa jana na rais huyo wa Marekani akisema kuwa, Bolton hafai tena kuwa kwenye serikali yake.

Trump aliandika katika mtandao wake wa Twitter kwamba, jana usiku nilimjulisha John Bolton kuwa kuanzia sasa White House haina haja na utumishi wake.

Rais wa Marekani ameongeza kuwa, mimi kama walivyo baadhi ya watu serikalini, tulikuwa tunapinga vikali misimamo na mapendekezo yake hivyo nimemtaka "John" ajiuzulu, naye amefanya hivyo leo.

Amesema, mshauri mpya wa usalama wa taifa wa Marekani atamtangaza wiki ijayo.

Hata hivyo John Bolton aliamua kumsuta waziwazi Trump kwa kusema kuwa aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu tangu Jumatatu usiku, lakini Trump alimwambia kuwa watazungumzia suala hilo jana Jumanne asubuhi.

John Bolton, mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani aliyetimuliwa serikalini

 

John Robert Bolton, ni miongoni mwa wafuasi wa mrengo wa misimamo mikali ya Kizayuni, kutokana chama cha Republican cha Marekani, na aliteuliwa na Trump kuwa mshauri wa usalama wa taifa tarehe 9 Aprili 2018.

Bolton ana misimamo mikali ya kuchochea vita hasa dhidi ya Iran na ni mmoja wa watu waliopanga na kumshawishi Trump ajitoe katika mapatano ya kimataifa ya nyuklia maarufu kwa jina la JCPOA.

Aidha Bolton ni miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa kigenge cha kigaidi cha MKO kilichofanya jinai kubwa dhidi ya wananchi na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags

Maoni