Sep 17, 2019 02:30 UTC
  • Indhari ya Waziri Mkuu wa Pakistan kuhusu vita vya nyuklia na India

Waziri Mkuu wa Pakistan amesema kuwa vita vya nyuklia vitashindwa kuepukika iwapo kutaanza vita kati ya nchi hiyo na India.

Imran Khan amezitahadharisha nchi zote duniani kuhusu vita vya nyuklia vinavyoweza kujiri kati ya Pakistan na India na kueleza kuwa taathira hasi za vita hivyo zitakuwa na madhara kwa wote; na kwa hiyo pande zote zinapasa kufanya juhudi ili kuyapatia ufumbuzi matatizo ya eneo la Kashmir linalodhibitiwa na India. Waziri Mkuu wa Pakistan ameongeza kuwa iwapo vita vitaanza kati ya India na Pakistan; mwisho wake utakuwa ni kuvurumishwa makombora ya nyuklia; jambo ambalo litapelekea kuangamizwa eneo zima. Serikali ya India imefunga njia zote kuelekea katika eneo la Kashmir na kuwazuia raia katika vifungo vya nyumbani tangu siku 42 zilizopita wakati ilipotangaza mamlaka ya kijeshi katika eneo hilo. Matamshi ya Imran Khan kwamba iwapo kutatokea vita baina ya Pakistan na India basi vita hivyo vitaishia katika kuvurumishwa makombora ya nyuklia zaidi ya kuwa ni ishara ya kuwa tayari nchi mbili hizo kukabiliana kijeshi; yametolewa kwa lengo la kuishawishi jamii ya kimataifa na khususan madola makubwa yaingilie kati mzozo wa Kashmir baada ya India kulifutia eneo hilo mamlaka ya kujiendeshea mambo yake lenyewe. Hatua hiyo imeshadidisha hali ya mgogoro katika uhusiano wa New Delhi na Islamabad. Pamoja na kuwa  India na Pakistan zinamiliki silaha za nyuklia lakini nchi mbili hizo zinafahamu vyema kwamba, katika mazingira ya sasa na kwa mujibu wa taratibu zilizopo katika mfumo wa kimataifa hakuna uwezekano wa kutumiwa silaha za nyuklia katika vita vyovyote vile vinavyoweza kutokea licha ya  kutoleana vitisho vya nyuklia. Ndio maana jamii ya kimataifa ikawa haizingatii sana tishio lolote la nyuklia linalotolewa na nchi moja dhidi ya nyingine.

Kwa kuzingatia hali hii ya mzozo wa muda mrefu iliyopo katika uhusiano wa India na Pakistan ya vitisho vya kushambuliana kwa silaha za nyuklia ambayo imeshika kasi kutokana na kupamba moto hali ya mvutano kati ya nchi mbili hizo au kutokana na  anga ya uchaguzi iliyochukua sura ya uzalendo wa kitaifa;  Narendra Modi Waziri Mkuu wa India pia akiwa katika kampeni za uchaguzi wa bunge la nchi hiyo mwezi Mei uliopita alizungumzia suala hilo katika mkutano mmoja wa kampeni na kukabiliwa na radiamali kali ya viongozi wa Islamabad. 

Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India
 

Kwa hiyo, hata kama kutajiri vita vya nyuklia baina ya India na Pakistan na vita hivyo kuzusha hofu kwa raia wa nchi zote mbili na hata kulitia wasiwasi eneo zima kwa ujumla, lakini viongozi wa New Delhi na Islamabad na nchi nyingine pia hawatilii maanani suala hilo kwa sababu muundo wa kimataifa uliopo hauandai mazingira ya kujiri jambo hilo.  

Katika hali ambayo baada ya eneo la Kashmir kufutiwa mamlaka ya kujiendeshea mambo yake yenyewe; stratejia kuu ya Pakistan ilikuwa ni kuifanya ya kimataifa kadhia ya Kashmir na kuyashawishi madola makubwa duniani na taasisi muhimu zenye taathira katika eneo na kimataifa kuiwekea India mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa ili ibadili msimamo wake kuhusu Kashmir; matamshi ya Imran Khan kuhusu ulazima wa jamii ya kimataifa kuzingatia taathira za vita kati ya Islamabad na New Delhi ambazo mwisho wake utakuwa ni mapigano ya nyuklia, yanatathminiwa kuwa ni katika juhudi zenye lengo la kuzivutia pande muhimu kimataifa ili kuwa na mchango na nafasi chanya katika kadhia ya eneo la Kashmir. 

Wakazi wa  Kashmir wakiandamana kulalamikia vifungo vya nyumbani kwa raia wa eneo hilo.  
 
Maoni