Sep 17, 2019 03:16 UTC
  • Baada ya kipigo cha ndege za Yemen, Trump naye kwa mara nyingine awadhalilisha viongozi wa Saudia

Licha ya kutambua vyema kwamba viongozi wa Saudi Arabia hivi sasa wanapitia kipindi kigumu baada ya pigo walilopata la ndege zisizo na rubani za Yemen katika vituo muhimu vya mafuta vya Saudia, lakini rais wa Marekani haoneshi kushughulishwa na hali hiyo ya viongozi wa Riyadh na amewataka walipie msaada wowote wa kijeshi watakaopewa na Marekani.

Televisheni ya Russia Today imemnukuu Donald Trump akisema katika mazungumzo yake na mrithi wa kiti cha ufalme wa Bahrain katika Ikulu ya Marekani, White House kwamba, Washington iko tayari kulinda usalama wa Saudi Arabia lakini kwa sharti kwamba viongozi wa Riyadh watoe fedha zaidi za kununua usalama huo.

Vile vile rais huyo wa Marekani ambaye anachojali yeye ni fedha tu kwa mara nyingine ametoa madai yasiyo na mashiko kwamba eti Iran imehusika na mashambulizi ya jeshi la Yemen katika taasisi za mafuta za Saudia lakini wakati huo huo amesema kuwa, nchi yake kamwe haina nia ya kuingia vitani na Iran.

Moro na moshi mzito katika taasisi za mafuta za Saudi Arabia baada ya kushambuliwa na droni za Yemen

 

Huko nyuma pia Donald Trump amewahi kuwadhalilisha mara kadhaa viongozi wa Saudi Arabia akiwaita ni ng'ombe tu wa kukamuliwa maziwa na kusema kuwa, utawala wa kifalme wa Saudia utaporomoka wiki mbili tu kama utakosa uungaji mkono wa Marekani.

Jumamosi alfajiri, ndege 10 zisizo na rubani za Yemen zilijibu jinai zinazofanywa na Saudia dhidi ya wananchi wa nchi hiyo, kwa kushambulia taasisi za mafuta za Buqayq na Khurais za shirika la taifa la mafuta la Saudi Arabia ARAMCO na kusababisha hasara kubwa kiasi cha kuilazimisha Riyadh kusimamisha nusu nzima ya uzalishaji wake wa mafuta wa kila siku.

Jeshi la Yemen na Kamati za Kujitolea za Wananchi wa Nchi hiyo zimewatahadharisha wageni na mashirika yao wakae mbali na maeneo nyeti ya Saudia kwani mashambulizi yanaendelea. 

Tags

Maoni