Sep 18, 2019 02:41 UTC
  • Rais wa Afghanistan anusurika katika shambulizi la bomu la Taliban

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan ameponea chupuchupu katika shambulizi la bomu lililojiri karibu na mkutano wake wa kisiasa katika mji wa Charikar, makao makuu ya mkoa wa Parwan kaskazini mwa Kabul.

Rais huyo ameripotiwa kuwa salama na kwamba hajajeruhiwa katika mripuko huo wa bomu wa jana Jumanne ambao umeua makumi ya watu. Msemaji wa timu ya kampeni ya rais huyo, Hamed Aziz amesema "Rais Ghani alikuweko kwenye eneo la tukio lakini yuko salama."

Naye Abdul Qasim Sangin, Mkuu wa Hospitali ya Parwan amenukuliwa akisema kuwa, watu 24 wameuawa katika shambulizi hilo, huku wengine zaidi ya 30 wakijeruhiwa.

Kundi la Taliban limekiri kuhusika na mripuko huo. 

Rais Ghani (kushoto) na wanachama wa kundi la Taliban

Wakati huohuo, Msemaji wa ofisi ya kisiasa ya kundi la Taliban iliyoko nchini Qatar amesema, ikiwa Marekani haitatekeleza ahadi na majukumu yake itabeba dhima ya kuendelea vita nchini Afghanistan.

Mashambulizi ya kigaidi yameshadidi nchini Afghanistan licha ya Marekani na waitifaki wake kutuma majeshi nchini humo tangu mwaka 2001 kwa kile kilichosemwa ni kwenda kupambana na ugaidi na kurejesha amani nchini humo.

Tags

Maoni