Sep 18, 2019 11:55 UTC
  • Katika mtazamo wa Kansela wa Ujerumani; Mwarubaini wa kupunguza mivutano Magharibi ya Asia ni kurejea kwenye JCPOA

Kwa mtazamo wa Umoja wa Ulaya na Troika ya umoja huo inayoundwa na Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yana mchango muhimu sana katika kulinda amani na usalama katika eneo la Magharibi ya Asia na katika uga wa kimataifa. Kwa mtazamo wa nchi za Ulaya, kujitoa Marekani katika JCPOA kumekuwa chanzo cha kujitokeza mivutano na hali ya wasiwasi katika Ghuba ya Uajemi na Magharibi ya Asia.

Kuhusiana na suala hilo, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesisitiza kuwa, kuna njia moja tu ya kupunguza mivutano katika eneo la Magharibi ya Asia, nayo ni kurejea kwenye makubalinao ya kimataifa ya nyuklia na kuyatekeleza makubaliano hayo. Merkel alitoa sisitizo jana Jumanne mjini Berlin, Ujerumani katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Mfalme Abdullah II wa Jordan. Alisema: Berlin inaamini kwa dhati kuwa makubaliano ya nyuklia tuliyofikia na Iran mwaka 2015 ndio muundo tunaopaswa kuurejea kwa ajili ya kupunguza mivutano. Kansela wa Ujerumani ameashiria ongezeko la kutia wasiwasi la mivutano katika eneo kufuatia mashambulio ya ndege zisizo na rubani yaliyofanywa na muqawama wa Yemen dhidi ya vituo vya mafuta vya Saudi Arabia, na akabainisha kuwa, daima amekuwa akiamini kwamba, njia ya ufumbuzi thabiti na wa kudumu itapatikana kupitia mazungumzo ya kisiasa. 

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani (kulia) na Mfalme Abdullah II wa Jordan

Lakini kinyume na mtazamo wa Kansela Merkel wa Ujerumani, msimamo na radiamali iliyoonyeshwa na Marekani baada ya shambulio hilo la karibuni ni ya uzushaji tuhuma na utoaji vitisho dhidi ya Iran. Kwa hakika serikali ya Trump ingali inaendelea kung'ang'ania msimamo wake potofu iliouchukua, wa kujitoa katika makubaliano ya JCPOA, ambao haujawa na matokeo mengine isipokuwa kuzidisha mivutano na kuvuruga uthabiti katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Kwa mtazamo wa Troika ya Ulaya pamoja na Umoja wa Ulaya, hatua ya Washington ya kujitoa katika JCPOA na vilevile kuvurugika au hata kuvunjika moja kwa moja makubaliano hayo ya nyuklia kutakuwa na taathira hasi za kiusalama. Nchi za Ulaya zinaitakidi kuwa, JCPOA ni mfano mzuri wa makubaliano ya pande kadhaa yanayoweza kuwa kigezo cha kufuatwa kwa ajili ya kutatua migogoro na mizozo mingine ya kimataifa.

Sisitizo la Kansela wa Ujerumani, ambayo ni nchi muhimu zaidi katika Umoja wa Ulaya kuhusu nafasi na mchango wa JCPOA katika kulinda amani na uthabiti kieneo na kimataifa linakinzana waziwazi na mtazamo wa serikali ya Trump kuhusu makubaliano hayo. Rais huyo wa Marekani amedai mara kadhaa kuwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hayadhamini maslahi na malengo ya Marekani na kimsingi hayawezi kuzuia maendeleo ya nyuklia ya Iran katika zama za baada ya JCPOA.

Kwa kutegemea madai ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba Iran inaendeleza kwa siri shughuli zake za nyuklia, mnamo mwezi Mei 2018, Trump alitangaza uamuzi wa kujitoa nchi yake katika makubaliano ya JCPOA; na kwa kutumia sera za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa, akaanza kutekeleza katika awamu mbili za miezi ya Agosti na Novemba vikwazo vikali dhidi ya Iran ambavyo havijawahi kushuhudiwa, mkazo mkubwa zaidi ukiwa ni kulenga sekta ya mafuta kwa kuhakikisha uuzaji mafuta wa Iran unasita kikamilifu hadi kufikia kiwango cha sifuri.

Vikwazo vikali vya kiuchumi ambavyo havijawahi kushuhudiwa pamoja na mashinikizo makali ya Washington vimeshadidisha mvutano baina ya Iran na Marekani, miongoni mwa athari za mivutano hiyo, yakiwa ni matukio yaliyojiri katika miezi ya karibuni katika Langobahari la Hormuz na Ghuba ya Uajemi. Serikali ya Trump imeamua kutekeleza sera za vitisho na mashinikizo dhidi ya Iran. Hata hivyo hatua zote zilizochukuliwa na Iran katika Ghuba ya Uajemi na Langobahari la Hormuz ni jibu la kujihami na kinga ya kukabiliana na hatua za vitisho zilizochukuliwa na Marekani. Kushadidi vikali mivutano kati ya Washington na Tehran kumezidi kuzitia wasiwasi nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zinaitakidi kuwa, kuna ulazima wa kutekelezwa siasa za kuondoa mivutano katika eneo hili. Ni kama alivyosema Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa  Jean-Yves Le Drian, kwamba: "Kuna haja ya kutekelezwa mkakati wa kuondoa mivutano. Kwa sababu hatua yoyote inayokinzana na uondoaji mivutano itakuwa na matokeo ya kusikitisha kwa eneo."  

Licha miito hiyo ya nchi za Ulaya, misimamo na hatua zilizochukuliwa na Marekani kuhusiana na matukio ya hivi karibuni katika eneo la Magharibi ya Asia hususan Ghuba ya Uajemi inakinzana na miito hiyo. Marekani imeongeza na kutuma idadi kubwa ya askari wake katika Ghuba ya Uajemi sambamba na kuanzisha muungano wa kimataifa wa baharini kwa lengo la eti kuvihakikishia usalama vyombo vya majini vinavyopita katika eneo hilo. Hata hivyo muungano huo hadi sasa haujaungwa mkono na zaidi ya nchi tatu. Lakini sambamba na hayo, baada ya mashambulio ya karibuni ya ndege zisizo na rubani dhidi ya vituo vya mafuta vya Saudia, Washington imeshadidisha lugha ya vitisho dhidi ya Iran. Hata hivyo Tehran imesisitiza kuwa imeshajiweka tayari kikamilifu kukabiliana na kitisho chochote kile kikiwemo hata cha utumiaji nguvu za kijeshi.../

Tags

Maoni