Oct 20, 2019 06:26 UTC
  • Wakati nchi za Ulaya zinapochoshwa na uadui wa Trump na kuamua kujibu vita vya kiuchumi

Viongozi wa Ulaya wamekasirishwa mno na vita vipya vya kiuchumi vilivyoanzishwa na rais wa Marekani, baada ya Donald Trump kutangaza ushuru mpya kwa bidhaa za nchi za Ulaya na hivyo kuingia katika vita vikubwa mno vya ushuru na waitifaki hao wa miaka mingi wa Marekani.

Hatua ya Marekani ya kuzichukulia hatua nchi za Ulaya kwa kuziwekea ushuru mpya kuanzia siku ya Ijumaa, imewakasirisha mno viongozi wa EU. Viongozi hao ambao sasa wamechoshwa na siasa za kiuadui za Marekani, nao wameamua kujibu kwa kuziongezea ushuru bidhaa za Marekani zinazoingia katika nchi za Umoja wa Ulaya. Marekani imeamua kuziongezea ushuru wa dola bilioni 7.5 bidhaa za Ulaya siku nne baada ya Shirika la Biashara Duniani kuiruhusu Washington kulipiza kisasi baada ya nchi za Ulaya kuamua kulipa ruzuku maalumu shirika la utengenezaji ndege la Airbus la nchi za Ulaya. 

Donald Trump ameamua kuzichukulia hatua nchi za Ulaya na kuongeza ushuru wa bidhaa za nchi hizo kutokana na EU kutenga ruzuku maalumu ya kulisaidia shirika la kutengeneza ndege la Airbus.

 

Anna Cecilia Malmström, kamishna wa masuala ya biashara wa Umoja wa Ulaya, juzi Ijumaa alielezea kusikitisha sana na uamuzi huo wa Marekani wa kuziongezea ushuru bidhaa za nchi za Ulaya kwa sababu tu nchi hizo zimetenga ruzuku maalumu ya kulisaidia shirika la ndege la Airbus na kusema kuwa, Umoja wa Ulaya hauna njia nyingine isipokuwa kujibu tu hatua hiyo ya Marekani. Hata hivyo hivi sasa nchi za Ulaya na Marekani zinasubiri uamuzi mwingine wa Shirika la Biashara Duniani kuona Umoja wa Ulaya utaiadhibu vipi Marekani kutokana na kulisaidia kifedha shirika lake la ndege la Boeing. Bruno Le Maire, waziri wa fedha wa Ufaransa amemtahadharisha Donald Trump kuhusu madhara ya siasa zake hizo za kiuadui dhidi ya nchi za Ulaya na kusema kuwa Umoja wa Ulaya utajibu tu hatua hiyo ya Marekani. Baada ya kuonana na Steven Mnuchin, waziri wa hazina wa Marekani, pambizoni mwa kikao cha kila mwaka cha Mfuko wa Fedha wa Kimataifa, Le Maire alisema, uamuzi huo wa Marekani utakuwa na matokeo mabaya ya kiuchumi na kisiasa.

Tangu mwezi Mei 2018 hadi hivi sasa, Marekani na nchi za Ulaya zimetumbukia kwenye vita vya ushuru baina yao na vita hivyo vilianzishwa na Marekani baada ya Donald Trump kuzipandishia ushuru bidhaa za feleji na aluminium zinazoingia Marekani kutoka barani Ulaya. Umoja wa Ulaya ulijibu uchokozi huo wa Donald Trump kwa kuzipandishia ushuru kwa asilimia 25 bidhaa za Marekani kama vile pikipiki zinazoingia barani humo kutoka Marekani. Hata hivyo mwezi Julai 2018, Trump na Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya, Jean-Claude Juncker walifikia makubaliano ya kusimamisha vita hivyo vya kibiashara baina ya pande mbili.

Shirika la kutengeneza ndege la Boeing la Marekani. Nchi za Ulaya zinasema zitaichukulia hatua za kinidhamu serikali ya Marekani kwa kulisaidia shirika hilo

 

Tab'an, Donald Trump hakuchelewa kutia ulimi puani na kukanyaga makubaliano hayo ya kusimamisha vita baina ya Marekani na Umoja wa Ulaya. Trump aliendelea kung'ang'ania msimamo wake wa kuziwekea ushuru mkubwa bidhaa za nchi za Ulaya kama vile magari na vipuri vyake na kufanya vita vya kibiashara baina ya pande hizo mbili marafiki wa muda mrefu viendelee kwa kasi kubwa zaidi. Ukweli ni kwamba katika vita vyake vya kiuchumi na kibiashara, Donald Trump hashughulishwi na rafiki au adui na mara kwa mara amekuwa akidai kuwa nchi za Ulaya zinaitumia vibaya Marekani kujinufaisha kibiashara. Kristalina Ivanova Georgieva-Kinova, mkurugenzi mpya wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa naye hivi karibuni alisema kuwa, vita vya kibiashara vilivyoanzishwa na Donald Trump vyenye thamani ya uchumi mzima wa Uswisi yaani karibu dola bilioni 700, vimeutia hasara uchumi wa dunia.

Nchi za Ulaya zinaamini kuwa, vita hivyo vya kibiashara vitapelekea kuzorota ustawi wa kiuchumi duniani na kuzusha anga mpya ya kutoaminiana. Watu wa kawaida ndio watakaodhurika kutokana na kupanda bei za bidhaa. Vile vile siasa mbovu za Trump zimeusababishia matatizo uchumi wa Ulaya. Ni jambo lililo wazi kwamba nchi za Ulaya zimeshachoshwa na siasa za kiuadui za Marekani na hapana shaka kwamba mizozo na ugomvi baina ya pande hizo mbili utaendelea kuwepo maadamu Donald Trump yuko madarakani huko Marekani.

Tags

Maoni