Oct 20, 2019 10:31 UTC
  • Sisitizo la Rais Erdoğan la Uturuki kuendelea kuwepo kijeshi huko Syria

Licha ya usitishaji vita uliofikiwa kati ya Marekani na Uturuki, lakini Rais Recep Tayyip Erdoğan amesisitiza kuwa, askari wa nchi yake wataendelea kusalia katika maeneo ya ar-Raqqah na Al Hasakah, kaskazini mashariki mwa Syria.

Katika uwanja huo, Rais Erdoğan amebainisha kwamba kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Washington na Ankara juu ya usitishaji vita wa muda mfupi huko Syria, askari wa Uturuki hawataondoka katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya Kiarabu ambayo yanadhibitiwa na askari wa nchi yake. Sambamba na kueleza kuwa hadi sasa bado kuna tofauti kati ya Washington na Ankara kuhusiana na upana wa eneo linalotajwa kuwa  'eneo salama' kaskazini mwa Syria, rais huyo wa Uturuki amesema eneo hilo litakuwa la umbali wa kilometa 32 ndani ya ardhi ya Syria, na sio 22. Uvamizi wa jeshi la Uturuki nchini Syria ulianza tarehe 9 mwezi huu, kwa amri ya Rais Erdoğan na kwa kisingizio cha kupambana na wanamgambo wa Kikurdi na harakati za kigaidi kaskazini mwa Syria, uvamizi ambao umelaaziniwa na serikali ya Damascus, nchi za eneo na dunia nzima kwa ujumla. Kufuatia mashinikizo ya kimataifa, Uturuki hatimaye imelazimika kusitisha uvamizi wake nchini Syria kwa kipindi cha masaa 120. Ni wazi kuwa, makubaliano ya Marekani na Uturuki juu ya uvamizi wa ardhi ya Syria, hayaungwi mkono na wananchi wala serikali ya Damascus.

Uvamizi wa jeshi la Uturuki katika ardhi ya Syria

Katika uwanja huo Rais Bashar al-Assad wa Syria sambamba na kutaka kuondoka askari wa Uturuki na Marekani katika ardhi ya nchi yake, amesisitizia udharura wa kupambana na wavamizi wa taifa hilo. Baadhi ya duru za kisiasa na serikali za eneo pia zimetilia shaka makubaliano yaliyofikiwa kati ya Ankara na Washington na namna ya utekelezwaji wake. Kwa mfano, serikali ya Russia inasema kuwa, Uturuki na Marekani zilitakiwa kuzingatia mtazamo wa serikali ya Damascus katika kipindi cha kujadiliwa operesheni za kijeshi kaskazini mashariki mwa Syria. Hivyo kwa kuzingatia mienendo hasi ya pande hizo, Moscow ina wasiwasi mkubwa kuhusiana na uwezekano wa kuwepo mchezo mchafu wa kisiasa kati ya Ankara na Washington dhidi ya Syria. Katika uwanja huo, Dmitry Peskov Msemaji wa serikali ya Russia ameyazungumzia makubaliano hayo kati ya Ankara na Washington kuhusiana na usitishaji operesheni za kijeshi za Uturuki kaskazini mwa Syria kwa masaa 120 na kusema: "Viongozi wa Russia wanatumai kwamba upande wa Uturuki utawasilisha kwa serikali ya Moscow maelezo ya lazima kuhusiana na suala hilo." Mienendo ya watawala wa Marekani inaonyesha kwamba wanajaribu kutumia kila mbinu ili kuweza kushibiti hali ya mambo nchini Syria.

Marais wa Uturuki na Marekani wanaokula njama dhidi ya Syria

Katika uwanja huo Vladimir Fetin, mtaalamu wa masuala ya kisiasa na mkuu wa kitengo cha Asia Magharibi katika taasisi ya utafiti wa kistratijia ya Russia anasema: "Usitishaji uvamizi wa kijeshi wa Uturuki nchini Syria, ulikuwa ukitarajiwa, hasa ikizingatiwa kwamba viongozi wa serikali ya Ankara walikuwa wanakabiliwa na mashinikizo kutoka kila upande." Aidha mtaalamu huyo wa masuala ya kisiasa na kistratijia wa Russia anafafanua kuwa: "Wamarekani wamefahamu kwamba huenda wakampoteza mshirika wao muhimu hususan kwenye Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi NATO. Hivyo wamekuwa wakitumia kila njia kwa ajili ya kuhitimisha mvutano ulioibuka katika uhusiano wa nchi mbili. Kwa kuzingatia hilo, kuna uwezekano kwamba ujumbe wa Marekani haukwenda Uturuki ukiwa mikono mitupu, bali uliwasilisha mapendekezo mazuri kwa serikali ya Ankara." Kiujumla tuanaweza kusema kuwa, usitishaji vita wa siku tano wa jeshi la Uturuki huko katika maeneo ya Wakurdi wa Syria, huenda ukawa ni matokeo ya mapatano yaliyofikiwa kati ya Ankara na Washington. Ni wazi kwamba raia wa Syria pamoja na Wakurdi wanaoishi nchi hiyo ndio waathirika wakuu wa mapatano hayo ya Marekani na Uturuki.

Maoni