Oct 21, 2019 02:48 UTC
  • Ukosoaji mkali wa Waziri Mkuu wa Russia kwa siasa za kibeberu za Marekani

Siasa za upande mmoja za Marekani ambazo zimeshika kasi katika kipindi cha uongozi wa Rais Donald Trump, zimeshadidisha mizozo duniani.

Kupitia nara ya 'Marekani Kwanza' Trump anadai kuwa siasa hizo za upande mmoja zitaifanya Washington kuongeze nguvu na kuwashinda washindani wake. Mwenendo huo wa Marekani umekabiliwa na ukosoaji mkali wa washindani wa Washington kimataifa hususan Russia, ambayo licha ya kuashiria ubeberu na utumiaji mabavu wa Washington katika kuzilazimisha nchi nyingine zikubali matakwa yake, imelaani vikali tabia hiyo. Katika uwanja huo Dmitry Medvedev, Waziri Mkuu wa Russia sambamba na kuashiria kuwa siasa za kigeni za Marekani zinazingatia tu maslahi binafsi ya kiuchumi na kijografia na pia tamaa ya Washington kwa ajili ya kutaka kudhibiti dunia ikiwemo Ulaya na eneo la Balkan, amesisitiza kuwa mwenendo huo umekuwa na madhara makubwa ambapo hata Ulaya imechoshwa na siasa hizo za Marekani. Medvedev amesem: "Marekani inafuatilia kuona maslahi yake ya kiuchumi na kijografia yanasonga mbele na hii leo suala hili liko wazi kwa kila mtu, ambapo ndilo linaunda msingi na nguzo ya siasa za kigeni za Washington....Kufikia sera hii ya Marekani imekuwa na madhara mengi kwa nchi nyingine, wakiwemo washirika wake wa Ulaya. Waathirika wakuu wa siasa hizo za kibeberu za Washington ni Ulaya, hususan eneo la Balkan. Nchi za Ulaya zimechoshwa na tamaa na siasa hizo za Marekani."

Marekani na Russia, pande zinazokabiliana

Hivi sasa Marekani imeingia katika makabiliano makali dhidi ya nguvu mbili kimataifa yaani Russia na China ambapo katika nyuga tofauti Washington imezisababishia changamoto kadhaa nchi hizo. Kwa sasa Russia inaandamwa na vikwazo vikali vya madola ya Magharibi hususan Marekani, vikwazo vinavyotekelezwa kwa visingizio tofauti. Lengo hasa la madola hayo ni kuilazimisha serikali ya Moscow ikubali matakwa yao. Marekani inazishinikiza nchi za Ulaya zipunguze kiwango cha uhusiano wao na Moscow na kutoshirikiana nayo katika miradi ya nishati. Katika uwanja huo mwezi Juni mwaka huu Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alisema kwamba alitaraji nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kulipa umuhimu suala la kujidhaminia usalama wao wa nishati na kwamba hivi karibuni Russia itaondolewa katika mfumo wa kuzidhaminia nishati nchi za Ulaya. Trump amekuwa akidai kuwa washindani na marafiki wa Marekani wamekuwa wakiitumia vibaya, hivyo anataka mabadiliko ya msingi yafanyike katika uwanja huo. Msimamo wa Trump una maana ya kuendelea kutwishwa nchi nyingine hususan washindani, maadui na hata marafiki wa Marekani matakwa ya serikali yake. Pamoja na hayo akthari ya viongozi wa nchi kubwa za dunia wakiwemo washirika wa Ulaya wa Washington wameonyesha wasi wasi wao kuhusiana na siasa za Rais Donald Trump na kusema kwamba siasa hizo zitazipelekea nchi nyingine za dunia kutokuwa na imani na Marekani na mwishowe kuitenga katika ngazi za kimataifa.

Trump na ubabe wake wa kutaka kuitawala dunia

Kwa mujibu wa Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa: Nara ya 'Marekani Kwanza' ndio ilimuingiza Trump White House, lakini hivi sasa mguu wake umekanyaga mbali zaidi na sasa anapiga nara ya 'Marekani Pekee.' Yaani kwamba Marekani iko katika vita na wote na katika mazungumzo ya pande mbili inasisitiza juu ya kuushinda upande wa pili." Suala muhimu katika uwanja huu ni kuchoshwa nchi za Ulaya na kupenda makubwa kwa Trump katika mambo yote. Kinyume na maslahi ya Ulaya, rais huyo wa Marekani hata anazitaka nchi za bara hilo pamoja na troika ya Ulaya, yaani Ufaransa, Uingereza na Ujerumani kujiondoa kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA kama alivyofanya yeye mwaka uliopita. Aidha bila ya idhini au bila ya kuwajulisha waitifaki wake wa Ulaya, rais huyo wa Marekani ameondoa askari wa nchi yake kaskazini mwa Syria na kuandaa mazingira ya kutekelezwa mashambulizi ya Uturuki katika eneo hilo. Bila kusahau kuwa hivi karibuni pia serikali ya Washington ilianzisha vita vya ushuru wa forodha dhidi ya Ulaya. Kwa utaratibu huo ni kwamba Marekani ambayo inazingatia tu maslahi yake binafsi ya kiuchumi na kisiasa katika uga wa kimataifa, si tu kwamba imewafanya waitifaki wake kuchoshwa na tabia hizo, bali inazidi kutengwa kimataifa siku hadi siku.

Tags

Maoni