Oct 22, 2019 08:09 UTC
  • Marekani yasema iko tayari kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Uturuki

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema Rais Donald Trump yuko tayari kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Uturuki iwapo 'italazimu'.

Mike Pompeo amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CNBC yaliyorushwa hewani jana Jumatatu na kubainisha kuwa, "Rais Trump amejiandaa kikamilifu na yuko tayari kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Uturuki ikibidi, lakini kwa sasa inafadhilisha nguvu za kidiplomasia."

Pompeo amekataa kufafanua kauli hiyo ya 'ikilazimu' lakini anasisitiza kuwa, Trump ndiye mwenye kauli ya mwisho kuhusu iwapo Uturuki imekiuka eti mstari mwekundu wa Marekani au la.

Hii ni katika hali ambayo, vikosi vya Uturuki vinatazamiwa kurejelea operesheni kikamilifu baada ya usitishaji vita wa muda uliofikiwa kati yake na Marekani kumalizika. Rais Recep Tayyip Erdoğan amesisitiza kuwa, askari wa nchi yake wataendelea kusalia katika maeneo ya ar-Raqqah na Al Hasakah, kaskazini mashariki mwa Syria.

Magari ya deraya ya Uturuki na Marekani nchini Syria

Uturuki ilianzisha operesheni ya kijeshi ya kuvamia ardhi ya Syria tarehe 9 Oktoba kwa madai ya kuanzisha "eneo salama" kusini mwa mpaka wake na Syria.

Ankara inasema, vikosi vya wapiganaji wa Kikurdi wanaoendesha shughuli zao katika eneo hilo ni magaidi wenye mfungamano na kundi la wanamgambo wa PKK ambalo limekuwa likipigania kuwa na eneo la kujiendeshea mambo yake ndani ya Uturuki tangu mwaka 1984.

 

 

Tags

Maoni