Oct 22, 2019 11:35 UTC
  • China: Marekani inakusudia kuanzisha mapinduzi ya rangi nchini kwetu

Waziri wa Ulinzi wa China sambamba na kukosoa ushadidishaji wa siasa za uingiliaji wa Marekani ndani ya nchi hiyo, amesema kuwa Washington inakusudia kuibua mapinduzi ya rangi ndani ya nchi hiyo.

Wei Fenghe ameyasema hayo katika kongamano la kimataifa mjini Beijing ambapo akiashiria hatua ya kupitishwa na wawakilishi katika bunge la Marekani mpango unaoitwa 'Demokrasia na Haki za Binaadamu mjini Hong Kong' ameongeza kuwa, Washington inatumia mbinu tofauti kuingilia masuala ya ndani ya China ili iibue mapinduzi hayo ya rangi. Waziri wa Ulinzi wa China amekosoa uingiliaji masuala ya ndani ya nchi nyingine, kuibua mapinduzi ya rangi na kuziondoa madarakani serikali halali na za kisheria kuwa ndilo lengo kuu la vita tofauti vinavyotekelezwa na Marekani duniani.

Wei Fenghe, Waziri wa Ulinzi wa China

Amesisitiza kuwa kamwe Beijing haitosalimu amri mbele ya mashinikizo ya kigeni na kwamba wale ambao wanataka kuingilia masuala ya ndani ya China, hawatofikia malengo yao. Kwa mara nyingine Wei Fenghe amewatahadharisha wale wanaotaka kujitenga na kuongeza kuwa China haitonyamazia kimya upenyaji wa kigeni pamoja na harakati za wanaotaka kujitenga eneo la Taiwan. Kongamano hilo la kimataifa litakalofanyika kwa muda wa siku tatu, lilianza Jumatatu ya jana kwa kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 70 za dunia. Katika kongamano hilo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewakilishwa na Mehdi Rabbani, Naibu Mkuu wa Majeshi ya nchi hii.

Maoni