Oct 23, 2019 02:43 UTC
  • Kubakia Uingereza katika njia panda ya Brexit

Mvutano kuhusu kujiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya mpango unaojulikana kama Brexit umegeuka na kuwa mjadala mkubwa na wa kila upande baina ya Bunge na serikali ya nchi hiyo.

Mvutano huo umekuwa mkubwa kiasi kwamba, siku ya Jumatatu, Bunge la nchi hiyo lilichukua hatua iliyozusha makelele ya kumzuia Waziri Mkuu Boris Johnson asiwasilishe kwa ajili ya kupigiwa kura katika Bunge hilo makubaliano yake mapya aliyofikia na Umoja wa Ulaya juu ya namna London itakavyojiondoa katika umoja huo. Hiyo ilikuwa mara ya pili ambapo Waziri Mkuu Boros Johnson alikuwa akitaka makubaloano yake na Umoja wa Ulaya yapigiwe kura na Bunge la Uingereza. Kwa mujibu wa makubaliano hayo mapya ambayo yanapingwa na akthari yya Wabunge wa nchi hiyo, Ireland ya Kaskazini kivitendo itabakia katika Jumuiya ya Forodha ya Umoja wa Ulaya na kwa muktadha huo, nchi hiyo itakuwa imejitenga na Uingereza katika uga wa kiuchumi.

Jambo hilo limewakasirisha hata Wabunge wa Uingereza wanaoafiki mpango wa nchi yao wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya (Brexit) na kuyatathmini makubaliano hayo kuwa mabaya hata kuliko yale ya Theresa May, Waziri Mkuu wa nchi hiyo aliyelazimika kujiuzulu.

John Bercow, Spika wa Bunge la Uingereza

John Bercow, Spika wa Bunge la Uingereza anasema: Kwa mujibu wa sheria haiwezekani kuwasilisha muswada mmoja Bungeni mara mbili, muswada huu uliwasilishwa Bungeni Jumamosi iliyopita ukiwa na hali hii hii ambapo yamepita masaa 48 huku muswada huo ukiwa haujafanyiwa marekebisho. Kwa msingi huo, muswada huu wa serikali hauwezi kupelekwa tena Bungeni na kujadiliwa.

Hatua hiyo ya Bunge la Uingereza inachukuliwa katika hali ambayo, Jumamosi iliyopita, pendekezo lililowasilishwa na Mbunge wa kujitegemea Oliver Letwin la kuongezwa muda wa Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya lilipasishwa kwa kura 322 za ndiyo dhidi ya 306 za hapana na kwa msingi huo kuifanya serikali isiweze kuwasilisha muswada wake Bungeni wa kuiondoa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya bila ya maafikiano ifikapo Oktoba 31.

Aidha kwa mujibu uamuzi wa Bunge la Uingereza, Waziri Mkuu Boris Johnson amelazimika kuliandikkia barua Baraza la Ulaya akiomba kuongezewa muda wa Brexit. Hii ni kkatika hali ambayo, Johnson na maafisa wa serikali yake, wangali wanasisitiza juu ya kuiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya katika muda uliopangwa yaani kufikia Oktoba mwezi huu.

Image Caption

Michael Gove, Waziri Mshauri wa Uingereza Katika Masuala ya Brexit ametangaza kuwa, licha ya kuwa Wabunge wamemlazimisha Waziri Mkuu kuomba muhula zaidi kutoka Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kutekeleza mpango wa kujiondoa Uingereza katika umoja huo, lakini Brexit itatekelezwa Oktoba 31, na Bunge haliwezi kubadilisha mtazamo, siasa na azma ya Boris Johnson.

John McDonnell, msemaji wa chama cha Leba katika masuala ya fedha ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: 

Johnson ni Waziri Mkuu ambaye hadi sasa amekuwa na muamala wa kiudhalili na Bunge na vyombo vya mahakama na hatua yake ya kitoto ya kukataa kutia saini barua, inaunga mkono dhana yetu mbaya daima dhidi yake kwamba, Johnson kutokana na kiburi na hali ya kujiona aliyonayo, amekuwa akitambua kama mtu aliye juu ya sheria ambaye hapaswi kuwajibishwa.

Endapo mchakato wa Uingereza wa kujitoa katika Umoja wa Ulaya utaakhirishwa tena, kuna uwezekano wa kuitishwa uchaguzi mwingine nchini Uingereza wa kumchagua Waziri Mkuu na hivyo kuanza tena mazungumzo kuhusiana na namna nchi hiyo inavyopaswa kujiondoa katika EU, mwenendo ambao utachukua muda na hivyo kuzidi kuongeza hali ya kutoeleweka hatima ya mambo mengi kisiasa, kiuchumi na kiusalama.

Katika siku za hivi karibuni kumeibuka utata katika uga wa siasa za Uingereza, madhara ya kiuchumi na kupungua kwa sarafu ya pauni hali ambayyo imezidisha malalamiko ya wananchi kiasi kwamba, katika kipindi cha siku mbili zilizopita zaidi ya wananchi 250,000 kupitia barua ya wazi wametaka kuitishwa tena kura ya maoni katika kipindi cha masaa 48 yajayo itakayoainisha hatima ya makubaliano ya Brexit.

Makabiliano kati ya Waziri Mkuu Boris Johnson na Bunge, kuongezeka ufa baina ya vyama vya siasa nchini Uingereza, kushadidi mashinikizo ya Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kutekelezwa Brexit, kubakia katika hali isiyoeleweka raia wengi wa Uingereza hususan katika uga wa kiuchumi na wasiwasi wa ukosefu wa usalama hususan katika mipaka yya Ireland ni mambo ambayo yameifanya Brexit kuwa kadhia isiyo na utatuzi. Inaonekana kuwa, siku chache hizi zilizobakia hadi kufikia tarehe 31 Oktoba, zitakuwa ngumu na zenye kuainisha mambo katika uga wa siasa za Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Tags