Oct 23, 2019 06:44 UTC
  • Badala ya ubabe na unyonyaji wa Magharibi, Russia yataka kuamiliana na Afrika kwa msingi wa maslahi ya pande mbili

Russia, ambayo ni moja ya madola makubwa duniani imeukosoa muelekeo na muamala wa Magharibi kwa bara la Afrika ambao siku zote huwa ni wa unyonyaji na utumiaji mabavu na badala yake inataka kustawisha uhusiano wake na nchi za bara hilo kwa msingi wa kuzingatia manufaa na maslahi ya pande zote mbili.

Katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na vyombo vya habari kwa mnasaba wa mkutano wa kiuchumi wa Russia na Afrika unaoanza leo Jumatano ya tarehe 23 Oktoba na kuendelea hadi kesho Alkhamisi Oktoba 24 katika mji wa bandari wa Sochi, Rais Vladimir Putin wa Russia amesisitiza kuwa, Moscow inalaani mchezo wa kijiopolitiki unaochezwa na baadhi ya nchi za Magharibi ili kuwa na satua na ushawishi barani Afrika kwa kutumia ghilba na vitisho; na mkabala na mwenendo huo iko tayari kushindana kisheria kwa ajili ya mashirikiano na nchi za Afrika yatakayozinufaisha pande zote mbili. Sambamba na hilo, Putin ameeleza matarajio aliyonayo kwa mkutano huo unaofanyika katika ngazi ya viongozi wa juu na vile vile ametahadharisha kuhusu hatari ya kujitokeza makabiliano ya kiuchumi barani Afrika kati ya madola makubwa. Aidha ametilia mkazo kupanuliwa na kustawishwa mashirikiano ya kijeshi na kiufundi pamoja na misaada ya kibinadamu ya Moscow kwa nchi za Afrika.

Rais Vladimir Putin wa Russia

Rais wa Russia anaitakidi kuwa, hivi sasa bara la Afrika limegeuka kuwa bara la fursa nyingi. Bara hilo lina utajiri mwingi wa maliasili huku masoko ya ndani pamoja na soko la watumiaji katika nchi za Kiafrika yakiendelea kupanuka. Pamoja na hayo, Wamagharibi wamekuwa na nafasi haribifu katika bara hilo. Kuhusiana na hilo Putin anasema: Tunashuhudia jinsi baadhi ya nchi za Magharibi zinavyoamiliana na nchi za Afrika kwa kutumia mashinikizo, ghilba na vitisho. Kupitia njia za aina hiyo, zinajaribu, tab'an kwa kutumia mbinu mpya, kurejesha satua na ubeberu wao kwa wanayoyaita makoloni yao ya zamani, bila kujali manufaa ya watu wa bara hilo. Zinafanya kila jitihada pia ili kuzuia kustawishwa uhusiano wa Russia na nchi za Kiafrika."

Tangu karne kadhaa nyuma hadi sasa, muelekeo wa Magharibi kuhusiana na bara la Afrika siku zote umekuwa ni wa kikoloni, kiunyonyaji na wa kujinufaisha na utajiri wa bara hilo, sambamba na kuwakandamiza wanaopigania uhuru na kujitawala kwake. Japokuwa katika zama za baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia nchi nyingi za Afrika zilijipatia uhuru, lakini madola ya Magharibi yameendelea kujipenyeza katika miundo ya kisiasa na kiuchumi na hata ya kijeshi ili kuweza kulinda na kuimarisha satua na ushawishi wao barani humo.

Pamoja na hayo, katika miaka ya karibuni na baada ya kutokea mabadiliko ya msingi katika kambi za kiuchumi duniani, sambamba na kujitokeza madola mapya yenye nguvu za kiuchumi, hisa ya nchi za Magharibi katika soko la biashara la nchi za Afrika imepungua, ambapo China, India na Brazil, nchi tatu wanachama wa kundi la kiuchumi la BRICS, zimekuwa washirika wakubwa wa kibiashara wa nchi za bara la Afrika. Hivi sasa Russia pia, kama zilivyo nchi zingine wanachama wa BRICS, inajitahidi kutafuta fursa na nafasi ya kujikita barani Afrika. Baada ya kusambaratika Urusi ya zamani, hadi mwishoni mwa muongo wa 2000,Russia, ambayo ni mrithi wa shirikisho hilo la kisovieti, haikuweza kuwa na nafasi muhimu katika bara la Afrika kutokana na kutingwa na matatizo kadhaa ya ndani pamoja na kupungua nguvu na uwezo wake. Hata hivyo katika muhula wa pili wa uongozi wa Putin, sambamba na kufufuka nguvu za kisiasa, kiuchumi na kijeshi za Russia, nchi hiyo sasa inafanya juhudi ili iwe na nafasi muhimu barani Afrika; ambapo mkutano wa kiuchumi wa viongozi wakuu wa Russia na Afrika huko mjini Sochi unafanyika katika muelekeo huo.

Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini, nchi tano wanachama wa kundi la BRICS

Ni kama alivyoeleza Putin mwenyewe ya kwamba: Leo hii uhusiano wa Russia na Afrika unaendelea kupanuka na kustawi, na misaada mbali mbali inatolewa na Russia pamoja na jamii ya kimataifa kwa bara hilo katika nyuga tofauti, ikiwemo ya kupunguza madeni ya nchi za bara hilo, kupambana na maradhi ya kuambukiza, kupambana na ugaidi, uhalifu ulioratibiwa, magendo ya mihadarati, kusuluhisha mizozo na kuzuia kutokea migogoro.

Kwa kuzingatia uwezo wa rasilimaliwatu na maliasili lilizonazo, pamoja na hazina kubwa ya nishati na madini, katika hali ya sasa bara la Afrika linaendelea kuongeza na kuimarisha hatua kwa hatua nafasi yake katika mlingano wa nguvu kimataifa na kuzidisha mvuto wa madola makubwa duniani kwa bara hilo. Jambo hili limeibua mchuano mkali baina ya madola hayo kwa ajili ya kuimarisha uwepo na ushawishi wao barani humo. Pamoja na hayo, itikadi iliyonayo Russia ni ya kuwa na ushindani wa kiushirikiano na nchi za Kiafrika.../

Tags

Maoni