Oct 23, 2019 07:43 UTC
  • Nusu ya wananchi wa Marekani waunga mkono kusailiwa Trump

Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa nchini Marekani unaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya wananchi wa nchi hiyo wanaunga mkono juhudi za wabunge wa chama cha Democrat za kumsaili Rais Donald Trump.

Uchunguzi huo mpya wa maoni uliotangazwa jana na televisheni ya CNN unaonyesha kuwa asilimia 50 ya wananchi wa Marekani wanaamini kuwa Rais wa nchi hiyo Donald Trump anapasa kusailiwa na kuondoka White House. Trump hivi sasa anapambana na kashfa mpya inayomkabili kwa jina la "Ukraine Gate." 

Taraifa za ufichuaji zilizotolewa hivi karibuni na duru isiyofahamika zinaeleza kuwa, mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu Trump aliwasiliana kwa simu na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na kumtaka ampatie taarifa ambazo zitachafua itibari na shakhsia ya Joe Baiden mgombea wa kiti cha urais mwaka 2020 nchini Marekani kwa tiketi ya chama cha Democrat na ambaye anatajwa kuwa ni mpinzani wake mkuu katika kinyang'anyiro hicho. 

Joe Biden, mpinzani mkuu wa Trump katika uchaguzi wa 2020
 

Imeelezwa kuwa, Trump aliahidi kuipatia Ukraine msaada wa kijeshi wa dola milioni 250 ili Kiev nayo ifanye uchunguzi kuhusu madai ya ufisadi yanayowakabili Biden na mwanae wa kiume. Kabla ya kuibulia kashfa hii, mchakato wa kumsaili Trump ulikuwa tayari umeanza kufuatia agizo la Nancy Pelosy Spika wa bunge la wawakilishi la Marekani. Hadi sasa wawakilishi wa bunge hilo wasiopungua 225 wameunga mkono kusailiwa Trump. Wademocrat wanaamini kuwa hatua zilizochukuliwa hadi hii leo na rais wa nchi hiyo zimekiuka pakubwa katiba ya Marekani.

Maoni