Oct 23, 2019 07:49 UTC
  • Uturuki na Russia zafikia makubaliano kuhusu kaskazini mwa Syria

Rais Vladimir Putin wa Russia na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyep Erdogan wamesaini makubaliano yenye vipengee 10 kuhusu hali ya usalama huko kaskazini mwa Syria baada ya mazungumzo ya masaa kadhaa katika mji wa Sochi nchini Russia.

Katika kipengee cha kwanza cha makubaliano hayo, Marais wa Russia na Uturuki wamesisitiza kuhusu kulindwa mshikamano na umoja wa ardhi yote ya Syria. Russia na Uturuki pia zimesisitiza kuhusu azma yao ya kupambana na ugaidi katika miundo yake yote na taathira zake. Kwa mujibu wa makubaliao hayo, vikosi vyote vya wanamgambo wa Kikurdi vitaondoka huko Manbij na Tal Rifaat kaskazini mwa Syria. 

Wanamgambo wa Kikurdi wakijiandaa kuondoka katika mji wa Manbij
 

Makubaliano hayo yanaeleza kuwa, kuanzia saa sita mchana Jumatano tarehe 23 Oktoba wanajeshi wa Syria na askari wa kulinda mipaka wa Syria watawasili upande wa Syria katika mpaka baina ya nchi hiyo na Uturuki ili kurahisisha kuondoka wanamgambo wa Kikurdi na silaha zao umbali wa kilomita 30 kutoka katika mpaka wa Uturuki na Syria; zoezi ambalo linapasa kuhitimishwa katika muda wa masaa 150 yajayo. 

Russia na Uturuki vile vile zimekubaliana kuendelea kutafuta njia za kisiasa ili kuhitimisha mgogoro wa Syria katika fremu ya mazungumzo ya Astana. Jeshi la Uturuki Jumatano tarehe 9 mwezi huu lilianzisha mashambulizi  ya siku nane kaskazini mwa Syria kwa amri ya Rais wa nchi hiyo Recep Tayyep Erdogan kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kuwafurusha wanamgambo wa kikurdi katika mpaka wa Syria na nchi hiyo; wanamgambo ambao wanatajwa na Ankara kuwa ni magaidi. Mashambulizi hayo yamesitishwa sasa kufuatia kufikiwa mapatano Alhamisi iliyopita kati ya Uturuki na Marekani ili kusimamisha vita kwa muda wa siku tano huko kaskazini mwa Syria. 

Maoni