Nov 14, 2019 09:41 UTC
  • Hatua mpya kuelekea kuuzuliwa Rais Trump wa Marekani

Mwezi mmoja na nusu baada ya kuidhinishwa uchunguzi wa kusailiwa na kumuuzulu Rais Donald Trump katika Bunge la Wawakilishi nchini Marekani sasa wabunge wameanza vikwazo vya wazi ,vinavyorushwa hewani moja kwa moja katika televisheni, kuhusu kashfa ya 'Ukrainegate' inayomkabili mtawala huyo wa Marekani.

William B. Taylor kaimu balozi wa sasa wa Marekani nchini Ukraine alikuwa mtu wa kwanza kutoa ushahidi katika kikao cha wazi katika kamati ya bunge la Kongresi ambayo inachunguza kashfa hiyo. Katika kikao hicho Taylor amesema: "Kwa Rais wa Marekani, maudhui ya kufanya uchunguzi dhidi ya mwana wa kiume wa Joe Biden ilikuwa muhimu zaidi kuliko hatima ya Ukraine."

Kabla ya ushahidi wa Taylor, Adam Schiff wa chama cha Democract ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Intelijensia ya Kongresi pia alisema Rudy Giuliani,  wakili binafsi wa Donlad Trump alikuwa anaongoza mtandao usio rasmi wa sera za kigeni na aliishinikiza Ukraine ili ifanye uchunguzi kuhusu shirika la Burisma Holdings la gesi la Ukraine."

Wakosoaji wa Trump wana matumaini kuwa,  ufichuaji huu utapelekea mchakato wa kuuzuliwa kwake uidhinishwe na Baraza la Wawakilishi na hatimaye kufikishwa katika Baraza la Senate.

Hii ni mara ya nne katika historia ya Marekani kufanyika vikao vya wazi kuhusu kuuzuliwa rais wa nchi.

William B. Taylor kaimu balozi wa sasa wa Marekani nchini Ukraine

Vikao vilivyopita viliwahusu  Andrew Johnson, Richard Nixon na Bill Clinton na kati ya hivyo vitatu, kikao kuhusu Nixon kilifanikiwa na hatimaye akalazimika kujiuzulu kama rais wa Marekani.

Kwa kuzingatia mazingira ya kisiasa yanayotawala hivi sasa mjini Washington, inatazamiwa kuwa Baraza la Wawakilishi ambalo linadhibitiwa na chama cha upinzani cha Democrat, litaidhinisha kuuzuliwa Trump. Lakini inaonekana itakuwa vigumu kwa Baraza la Senate, kuidhinisha kuuzuliwa Trump kwa sababu linadhibitiwa na chama tawala cha Republican. Maseneta wanapaswa kupitisha kwa thuluthi mbili pendekezo hilo la kumuuzulu Trump. Maseneta 45 wa chama cha Democrat na wawili wa kujitegemea na wengine 20 wa chama cha Republican wanapaswa kuidhinisha pendekezo la kumlazimu Trump ajiuzulu ili kufanikisha hatua hiyo.

Richard Nixon (kushoto) na Donald Trump

Hii ni katika hali ambayo, wakati wa kutaka kuanza mchakato wa kumuuzulu Trump, Warepublican hawakuunga mkono chama cha Democrat na fauka ya hayo, wanachama wawili wa chama cha Democrat walipinga mchakato huo wa kuanza uchunguzi dhidi ya Trump. Suala hili limempelekea Trump apate utulivu wa wastani kuhusu matokeo ya mchakato huo wa kumuuzulu. Baada ya Baraza la Wawakilishi kuanza kusikiliza ushahidi wa wazi dhidi ya Trump na televisheni za Marekani kurusha kikao hicho moja kwa moja, Trump aliwahutubia waandishi habari na kusema hakutazama kikao hicho katika televisheni.

Pamoja na hayo, iwapo  Wademocrat hawatafanikiwa  kumuuzulu Trump,  wana matumaini kuwa  ufichuaji unaoendelea utapelekea uwezekano wake wa kuchaguliwa katika uchaguzi wa rais mwakani kupungua.

Kinyume na kesi tatu zilizotangulia za kuuzuliwa marais wa Marekani, kesi hii imeanza wakati uchaguzi wa rais unakaribia. Kwa kuzingatia kuwa uchunguzi wa maoni unaashiria kupungua sana umashuhuri wa Trump miongoni mwa Wamarekani, na pia kupungua kura za Warepublican katika uchaguzi wa hivi karibuni wa majimboni, Wademocrat wanajitahidi kumpkonya Trump kura za wapiga kura huru na hata baadhi ya Warepublican waliokuwa wakimuunga mkono ili kwa njia hiyo ashindwe katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Novemba mwakani. 

Pamoja na hayo inabidi tusubiri tuone iwapo mkakati huu wa Wademokrat utafanikiwa au la na hilo litategemea pia ufichuzi zaidi katika kashfa ya Ukrainegate.

Maoni