Nov 15, 2019 01:24 UTC
  • Suu Kyi afunguliwa mashtaka kwa mara ya kwanza kwa jinai dhidi ya Wislamu wa Myanmar

Makundi ya kutetea haki za binadamu huko Amerika ya Latini yamewasilisha kesi dhidi ya Aung San Suu Kyi Mshauri wa ngazi ya juu wa serikali ya Myanmar na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la nchi hiyo kwa tuhuma za kuhusika na jinai na uhalifu uliofadhiliwa na serikali ya nchi hiyo dhidi ya Waislamu wa kabila la waliochache la Rohingya.

Wanaharakati wa makundi hayo ya kutetea haki za binadamu wamesema katika kesi iliyofunguliwa nchini Argentina kwamba, Suu Kyi na serikali yake wana mchango katika maangamizi ya kizazi na mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Rohingya kwa kushindwa kulaani ukandamizaji uliokuwa ukifanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya jamii hiyo na pia kwa kulisadia kuficha jinai na uhalifu huo.

Jeshi la Myanmar likichoma moto nyumba za Waislamu wa Rohingya 
 

Mashtaka hayo yaliyoongozwa na Tomas Ojea mwanasheria wa masuala ya haki za binadamu yaliwasilishwa kwa mujibu wa kipengee cha sheria ya kimataifa inayosema kuwa, baadhi ya vitendo kama jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu vinatisha sana kiasi kwamba si makhsusi kwa nchi moja tu, kwa msingi huo vinaweza kufunguliwa mashtaka sehemu yoyote ile.

Ojea ambaye alikuwa kaimu wa ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu nchini Myanmar kati ya mwaka 2008 na 2014 amesema kuwa, kesi hiyo inayoungwa mkono na makundi mawili ya haki za binadamu ya nchini Argentina inataka kufikishwa mahakamani viongozi wa ngazi ya juu wa masuala ya kijeshi na kisiasa akiwemo Mkuu wa Jeshi la Myanmar Aung Hlang na Aung San Suu Kyi kutokana na tishio la maangamizi ya Waislamu wa Rohingya.

Mwaka jana Shirika la Amnesty International lilisema kuwa maafisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Myanmar wanapaswa kushtakiwa katika Mahakama ya ICC kwa kutenda jinai dhidi ya binadamu dhidi ya Waislamu wa Rohingya. Waislamu zaidi ya 730,000 wa jamii ya Rohingya  wamekimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh kufuatia mauaji na ukandamizaji ulioongozwa na jeshi la Myanmar dhidi yao zilizoshadidi mwaka 2016.  

Tags

Maoni