Nov 15, 2019 04:44 UTC
  • Waislamu leo wanaadhimisha maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume SAW na Imam Ja'afar Swadiq AS

Waislamu leo wanaadhimisha maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa mbora wa viumbe Mtume Muhammad SAW pamoja na mjukuu wake Imam Ja'afar bin Muhammad al-Swadiq AS.

Wananchi wa maeneo mbalimbali hapa nchini Iran Mashia kwa Masuni wamepamba mitaa yao kwa maua na taa katika maadhimisho ya kuzaliwa Mtume wa Mwisho na mbora wa viumbe Muhammad SAW.

Ushiriki wa Waislamu wa Kishia na Kisuni nchini Iran katika sherehe ya maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume SAW unadhihirisha umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 1494 iliyopita kwa mujibu wa nukuu za maulama wengi wa Kiislamu, alizaliwa Mtume Muhammad (saw) katika mji mtakatifu wa Makka. Baba yake, Abdullah alifariki dunia kabla ya kuzaliwa Mtume, na mama yake Mtume yaani Amina binti Wahab, alifariki dunia mtukufu huyo akiwa na umri wa miaka sita.

Aidha siku kama ya leo ya terehe 17 Rabiul Awwal mwaka 83 Hijiria alizaliwa pia mjukuu wa mtukufu huyo Imam Ja'far Swadiq (as) katika mji mtakatifu wa Madina. Kipindi cha maisha yake kilikuwa zama za kuchanua elimu na maarifa, tafsiri ya Qur'ani na kusambaa elimu mbalimbali.

Kwa minasaba hii miwili adhimu Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa Waislamu wote duniani hususan wafuasi wakweli wa Mtume SAW na wapigania haki na uadilifu kote ulimwenguni.

Tags

Maoni