Nov 16, 2019 02:44 UTC
  • Morales aomba msaada wa UN na Papa Francis, akisisitiza angali ni rais halali wa Bolivia

Rais wa Bolivia aliyejiuzulu ameuomba Umoja wa Mataifa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis waingilie kati kupatanisha mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo.

Katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa nchini Mexico aliko uhamishoni, Evo Morales amesema, yeye angali ni rais halali wa Bolivia kwa sababu bunge la nchi hiyo halijakubali kujiuzulu kwake.

Morales ameongeza kuwa, amepokea taarifa kwamba baadhi ya vikosi vya jeshi la Bolivia vimekusudia kuasi dhidi ya maafisa wa jeshi hilo waliomlazimisha yeye ajiuzulu.

Rais huyo wa Bolivia aliyejiuzulu ameendelea kutoa mwito wa kuwepo utulivu na kufanyika mazungumzo nchini humo.

Rais wa Bolivia aliyejuizulu Evo Morales (wa pili kulia ) mara baada ya kuwasili uhamishoni nchini Mexico

Kufuatia kushadidi malalamiko, fujo na machafuko yaliyosababishwa na wapinzani pamoja na uingiliaji wa Marekani katika uchaguzi wa rais wa Bolivia uliofanyika tarehe 20 Oktoba, ambapo rais wa wakati huo Evo Morales aliibuka mshindi, mnamo tarehe 10 ya mwezi huu wa Novemba, kiongozi huyo alilazimika kujiuzulu kutokana na mashinikizo ya jeshi.

Baada ya kukabiliwa na hatari ya kuuawa kutokana na vitisho na vitendo vya ukatili vilivyofanywa na wafanyamapinduzi, siku ya Jumanne ya tarehe 12 Novemba, Morales alielekea Mexico baada ya serikali ya nchi hiyo kukubali kumpa hifadhi ya kisiasa.../

Maoni