Nov 16, 2019 06:10 UTC
  • Sisitizo la Marekani la kuvunja kikamilifu mkataba wake na Uturuki kuhusu ndege za kivita za F-35

Uhusiano wa Marekani na Uturuki haujatengenea tangu mwaka 2016 baada ya kutokea jaribio la mapinduzi nchini Uturuki na hasa kitendo cha Marekani cha kukataka kumkabidhi kwa Uturuki, Fethullah Gülen, anayetuhumiwa na Ankara kuwa muhusika mkuu wa jaribio hilo la mapinduzi.

Jambo jingine lililopelekea kuzidi kuharibika uhusiano wa nchi hizo mbili, ni hatua ya Uturuki ya kununua mfumo wa S-400 wa kujilinda na mashambulizi ya makombora kutoka kwa Russia, suala ambalo limepingwa vikali na Marekani. Washington ilitoa vitisho vingi kwa Ankara kabla haijanunua mfumo wa S-400 kutoka Russia lakini vitisho hivyo vyote havikuizuia Uturuku kununua mfumo huo wa kisasa wa kujilinda na mashambulizi ya makombora. Hatua iliyochukuliwa na Marekani baada ya hapo ni kuvunja mkataba wake na Ankara katika suala zima la ndege za kivita za F-35.

Mfumo wa makomborta wa S-400 wa Russia ukiwasili Uturuki

 

Hata hivyo hiyo haikuwa na maana ya kuvunjika kikamilifu uhusiano baina ya Marekani na Uturuki. Hii ni kusema kuwa, safari ya Rais Recep Tayyip Edrogan wa Uturuki huko Marekani imefanyika kwa lengo la kutafuta njia za kupunguza mivutano baina ya pande mbili na kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wao wa kiuchumi na kibiashara. Hata hivyo inaonekana kuwa safari hiyo ya rais wa Uturuki nchini Marekani imeshindwa kuondoa mzozo uliopo baina ya pande mbili. Licha ya ahadi za rais wa Marekani, Donald Trump kwa Erdogan baada ya kuonana viongozi hao wawili katika Ikulu ya White House, tarehe 13 mwezi huu wa Novemba, ahadi ambazo ni pamoja na kuweko muamala wa kiuchumi wa dola bilioni 100 baina ya nchi mbili, lakini hakuna yeyote mwenye yakini kuwa Trump atatekeleza kweli ahadi zake hizo.

Licha ya Trump kutoa ahadi hizo, lakini Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imetangaza kuwa, imepata sehemu nyingine ya kuzalishia vipuri vyote vya ndege za kivita za F-35 nje ya Uturuki. Generali Eric Fick, mkurugenzi wa mpango wa uzalishaji wa ndege za F-35 wa Marekani alisema wakati mazungumzo ya marais wa nchi yake na Uturuki yakiendelea kwamba Uturuki imeondolewa kikamilkifu kwenye mradi wa F-35 na kwamba utekelezaji wa agizo hilo utaanza rasmi mwezi Machi 2020. Hivi sasa Marekani imepunguza mno uzalishaji wa vipuri vya F-35 huko Uturuki kutoka vipuri 1000 hadi 12 tu na tayari imeshapata nchi nyingine ya kuzalisha vipuri hivyo. Bi Ellen Lord, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Marekani katika masuala ya ununuzi na kuhifadhi bidhaa amesema kuwa, licha ya kwamba vipuri vilivyokuwa vikizalishwa nchini Uturuki vilikuwa vizuri mno, lakini Marekani imeamua kutafuta nchi nyingine ya kuzalisha vipuri hivyo na kwamba uzalishaji wa ndege za F-35 hautokwamishwa na mabadiliko hayo. Matamshi hayo yalitolewa kujibu taarifa zilizosema kuwa Trump amemtaka tena Erdogan asinunue mfumo wa makombora wa S-400 kutoka Russia ambapo sehemu fulani ya mfumo huo ilikabidhiwa Uturuki mwezi Julai mwaka huu wa 2019.

Marais wa Marekani na Uturuki mjini Washington

 

Mara baada ya mazungumzo yake na Trump, Erdogan alidai kuwa ameona rais huyo wa Marekani ana mtazamo mzuri zaidi kuhusu ushirikiano wake na Uturuki. Licha ya kutolewa matamshi hayo, lakini suala muhimu zaidi hapa ni kwamba, hata tukijaalia kwamba Trump ana mtazamo mzuri kuhusu suala hilo, lakini muundo wa utawala nchini Marekani ambao nguzo yake kuu ni Baraza la Congress, hauwezi kukubaliana na uamuzi wa Uturuki wa kununua mfumo wa makombora wa S-400 kutoka Russia kama ambavyo pia Baraza la Congress la Marekani linapinga vikali uvamizi wa Uturuki katika maeneo ya kaskazini mwa Syria yaliyokuwa yanadhibitiwa na vibaraka wa Marekani. Msimamo wa Baraza la Congress la Marekani kwa serikali ya Uturuki ni mkali sana. Tarehe 30 Oktoba mwaka huu, baraza hilo lilipasisha azimio dhidi ya Ankara na kutambua rasmi kuwa utawala wa Othmania wa Uturuki uliwaua kwa umati Waarmenia mwaka 1915. Wabunge 305 wa Marekani walilipigia kura ya ndio azimio hilo ambalo lilipingwa na wabunge watatu tu. Baraza hilo la Congress limepasisha azimio jingine linalomtaka Donald Trump aiwekee vikwazo Uturuki kutokana na Ankara kulivamia eneo la kaskazini mwa Syria. Azimio hilo lilipasishwa na wabunge 403 na kupingwa na wabunge 16 tu, suala ambalo linazidi kuonesha kuwa mzozo baina ya Uturuki na Marekani hauwezi kutatuliwa kwa mazungumzo ya masaa machache ya marais wa nchi hizo mbili, kama ambavyo pia jambo hilo linazidi kuthibitisha kuwa ahadi zilizotolewa na Trump kwa Erdogan  hazina dhamana yoyote ya kutekelezwa.

Tags

Maoni