Nov 16, 2019 11:17 UTC
  • Marekani yatishia kuiwekea vikwazo Misri kwa kununua ndege za kivita za Russia

Mitazamo ya upande mmoja ya Marekani na juhudi za nchi hiyo za kuimarisha ubeberu wake duniani, ambazo zimepata kasi kubwa katika utawala wa Rais Donald Trump, imechukua muelekeo mpya ambao ulikuwa haujawahi kushuhudiwa huko nyuma.

Moja ya mifano ya wazi ya mitazamo na siasa hizo za upande mmoja za serikali ya Trump ni kuziainishia majukumu nchi waitifaki au washirika wa karibu wa Marekani kuhusiana na masuala ya ulinzi, usalama na ununuzi wa silaha. Marekani inaingilia wazi na bila haya masuala hayo ambayo yanahesabika kuwa moja ya misingi muhimu ya kujitawala nchi yoyote ile. Katika uwanja huo, Marekani imeitishia Misri kwamba itaiwekea vikwazo bila kusita iwapo itaendelea kusisitiza kununua ndege za kisasa za kivita za Sukhoi-35 kutoka Russia. Onyo hilo limetolewa katika barua iliyoandikwa na Mike Pompeo na Mark Esper, Mawaziri wa Mambo ya Nje na wa Ulinzi wa Marekani kwa utaratibu kwa Waziri wa Ulinzi wa Misri. Katika barua hiyo, mawaziri wawili hao wa Marekani wametishia kwamba iwapo Misri haitasimamisha ununuzi huo wa ndege za Russia, Washington itaiwekea vikwazo bila kusita. Mkataba wa ununuzi wa ndege hizo ulitiwa saini mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2018 na zinatazamiwa kukabidhiwa Misri kuanzia 2020. Ndege hizo zinatazamiwa kuchukua nafasi ya ndege aina ya  Mig-21 za Russia na J-7 za China. Marekani ambayo inadhibiti soko la mauzo ya silaha duniani inawazuia washirika na waitifaki wake kununua silaha za Russia ili ipate fursa ya kuendelea kuhodhi na kudhibiti soko hilo. Ni kutokana na siasa hizo za kimaslahi ndipo Marekani ikatoa onyo kwa Misri na kuitaka inunue ndege zake za kivita badala ya kununua za Sukhoi kutoka Russia.

Ndege ya kivita ya Russia aina ya Sukhoi-35

Hii si mara ya kwanza kwa Marekani kutishia kumuwekea vikwazo mmoja wa washirika wake kwa kutaka kununua silaha za Russia. Kwa kuzingatia azma ya Uturuki na India, washirika wengine wa Marekani, ya kutaka kununua mfumo wa makombora wa S-400 wa Russia, serikali ya Trump imetoa onyo kali kwa nchi hizo na kuzitaka zisimamishe mara moja ununuzi wa mfumo huo wa makombora.

Baada ya Marekani kuitaka Uturuki isinunue mfumo huo wa makombora wa S-400 kutoka Russia na hata kutekeleza baadhi ya vitisho dhidi ya nchi hiyo vikiwemo vya kuiondoa katika mpango wa ndege za kizazi cha tano za F-35, Washington imekuwa ikizidisha mashinikizo dhidi ya India na kutishia kuiwekea vikwazo iwapo haitatii amri yake ya kusimamisha ununuzi wa mfumo huo wa makombora wa S-400. Kwa mujibu wa sheria za Marekani, nchi hiyo inaruhusiwa kuiwekea vikwazo nchi yoyote ambayo itakuwa na uhusiano wa kiulinzi au habari za siri za na Russia. Kwa msingi huo Marekani imesema kuwa ununuzi wa India wa mfumo wa makombora wa S-400 kutoka Russia utahatarisha ushirikiano wa kiulinzi wa New Delhi na Washington. Kupitia siasa hizo, Marekani inataka kuifukuza Russai katika soko muhimu la silaha la India.

Marekani pia inatishia kuiwekea vikwazo India kwa kununua mfumo wa makombora wa S-400

Kwa mujibu wa Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, vikwazo vya Marekani dhidi ya Russia vinatekelezwa kwa shabaha ya kuifukuza nchi hiyo katika soko la silaha na nishati ulimwenguni. Marekani inaitazama Russia kuwa mpinzani wake mkuu katika soko la mauzo ya silaha duniani. Ni kwa msingi  huo ndipo mashirika ya utengenezaji silaha ya Russia yakawekewa vikwazo vipya na Marekani ili kupunguza shughuli zao za kawaida katika masoko ya silaha duniani. Pamoja na hayo lakini Uturtuki na India zingali zinasisitiza nia yao ya kununua mfumo wa makombora wa S-400 kutoka Russia. Bila shaka jambo hilo linathibitisha wazi azma ya nchi mbili hizo ya kukabiliana na siasa za upande mmoja na mabavu za Marekani na wakati huo huo kusisitiza juu ya siasa zao huru kuhusiana na suala la ulinzi na ununuzi wa silaha. Inatazamiwa kuwa Misri nayo itachukua msimamo kama huo wa kukabiliana na vitisho vya vikwazo vya Marekani kuhusiana na ununuzi wake wa ndege za kivita za Russia aina ya Sukhoi-35 na hivyo kusisitiza juu ya kujitawala kwake katika masuala yanayohusiana na ulinzi na silaha.

Tags

Maoni