Nov 19, 2019 02:40 UTC
  • Marekani yaikataza Misri kushirikiana na Russia, yaendelea kutoa vitisho dhidi ya Cairo

Kwa mara nyingine Marekani imetoa vitisho vikali kwa Misri kutokana na uamuzi wake wa kununua ndege aina ya Sukhoi-35 kutoka Russia.

Clark Cooper, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika masuala ya kisiasa na kijeshi alisema jana (Jumatatu) kwamba, hatua ya Misri ya kuamua kununua ndege kutoka kwa Russia kutafanya Marekani iiwekee vikwazo vikali Cairo na kutahatarisha manunuzi ya silaha za Marekani katika siku za usoni. Naibu huyo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema kuwa, Misri inatambua vyema hatari za hatua yake ya kununua ndege za kivita kutoka Russia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo

 

Onyo hilo jipya la Marekani dhidi ya Misri limetolewa katika hali ambayo, hivi karibuni Mike Pompeo na Mark Esper, Mawaziri wa Mambo ya Nje na wa Ulinzi wa Marekani walimwandikia barua Waziri wa Ulinzi wa Misri kutoa vitisho hivyo hivyo. Katika barua hiyo, mawaziri hao wawili wa Marekani walitishia kwamba iwapo Misri haitasimamisha ununuzi huo wa ndege za Russia, Washington itaiwekea vikwazo bila kusita. 

Mkataba wa ununuzi wa ndege hizo ulitiwa saini mwishoni mwa mwaka uliopita wa 2018 na zinatazamiwa kukabidhiwa Misri kuanzia 2020. Ndege hizo zinatazamiwa kuchukua nafasi ya ndege aina ya  Mig-21 za Russia na J-7 za China. Marekani ambayo inadhibiti soko la mauzo ya silaha duniani inawazuia washirika na waitifaki wake kununua silaha za Russia ili ipate fursa ya kuendelea kuhodhi na kudhibiti soko hilo. Ni kutokana na siasa hizo za kimaslahi ndipo Marekani ikatoa onyo kwa Misri na kuitaka inunue ndege zake za kivita badala ya kununua za Sukhoi kutoka Russia.

Tags

Maoni