Nov 20, 2019 12:48 UTC
  • Kituo cha Ron Paul Marekani: CIA imehusika katika kuchochea ghasia nchini Iran

Mtendaji Mkuu wa Kitivo cha Kimarakeni cha Ron Paul amefichua kwamba, Shirika la Ujasusi la Marekani CIA lilikuwa na nafasi kubwa katika kuchochea ghasia za hivi karibuni nchini Iran.

Daniel Mc Adams ameyasema hayo leo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya RT ya nchini Russia kuhusiana na machafuko na ghasia za hivi karibuni nchini Iran na kubainisha kwamba, matukio ya hivi karibuni nchini Iran hayakutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, bali ni ghasia ambazo zilitokana na uchochezi wa Marekani chini ya usimamizi wa Shirika la Ujasusi la Marekani CIA. Daniel Mac Adams ametoa mfano kwa kuashiria kundi la kigaidi la Munafiqin (MKO) ambalo linashirikiana moja kwa moja na Marekani katika kutekeleza jinai nchini Iran na kusema kuwa, kwa kiasi kikubwa machafuko kama hayo yamekuwa yakiratibiwa na CIA katika serikali ya Rais Donald Trump ambapo tangu mwaka uliopita jukumu lake lilikabidhiwa Michael D'Andrea, mmoja wa maafisa wa ngazi za juu wa shirika hilo na ambaye pia anajulikana kwa lakabu ya 'Ayatullah Mike.'

Daniel Mc AdamsMtendaji Mkuu wa Kitivo cha Kimarakeni cha Ron Paul

Kabla ya hapo pia gazeti la New York Times liliandika habari ambayo ilikabiliwa na radiamali nyingi kuhusiana na mpango ulio nyuma ya pazia ambao uliratibiwa na Michael D'Andrea ndani ya Shirika la Ujasusi la Marekani CIA, kupitia uungaji mkono wa Saudi Arabia na Imarati kwa lengo la kuibua ghasia na machafuko nchini Iran. Aidha Jumapili jioni ikulu ya Marekani White House, ilitoa taarifa ya uingiliaji ambapo sambamba na kukariri madai yake bandia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ililiunga mkono kundi dogo la watu waliofanya ghasia kwa kisingizio cha kupanda bei ya mafuta na kuvuruga utulivu wa miji kadhaa hapa nchini, ambapo waliharibu mali nyingi za umma.

Maoni