Nov 21, 2019 01:05 UTC
  • Makabiliano ya mitazamo katika mdahalo wa kwanza wa uchaguzi wa Uingereza kati ya Johnson na Corbyn

Uga wa siasa za Uingereza baada ya bunge la nchi hiyo kuafiki kufanyika uchaguzi wa kabla ya wakati tarehe 12 ya mwezi ujao wa Desemba, sasa umegeuka kuwa ulingo wa mchuano mkali kati ya vyama viwili vikuu vya siasa vya Wahafidhina na Leba wa kuvutia uungaji mkono wa wapigakura, huku kila chama kikijikakamua kubainisha sera na misimamo yake ili kuweza kuwa nafasi ya juu zaidi mbele ya wananchi.

Mdahalo wa kwanza wa uchaguzi kati ya Waziri Mkuu Boris Johnson ambaye ni kiongozi wa chama cha Wahafidhina na Jeremy Corbyn, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Leba, ulifanyika juzi Jumanne usiku tarehe 19 ya mwezi huu wa Novemba. Katika mdahalo huo uliosimamiwa na kanali ya televisheni ya ITV, viongozi hao wa vyama vya Wahafidhina na Leba walichuana vikali katika kubainisha mitazamo yao juu ya masuala mbali mbali ikiwemo Brexit, masuala ya kiuchumi, Huduma ya Taifa ya Afya (NHS) n.k.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson (kulia) na kiongozi wa chama cha Leba Jeremy Corbyn

Pamoja na hayo, moja ya masuala muhimu zaidi na ambalo bila shaka linawakereketa mamilioni ya Waingereza ni mustakabali wa mfumo wa Huduma ya Taifa ya Afya wa nchi hiyo. Moja ya maudhui iliyogusa mdahalo wa Johnson na Corbyn kuhusu suala hilo ni kwamba, yupi kati ya wawili hao ambaye, ikiwa atashinda katika uchaguzi, atakuwa na mipango bora zaidi ya kuendesha mfumo huo wa Huduma ya Taifa ya Afya? Jeremy Corbyn anamtuhumu Boris Johnson anayeungwa mkono na Rais Donald Trump wa Marekani kwamba, ana nia ya 'kuuza mfumo huo wa Huduma ya Taifa ya Afya wa Uingereza kwa mashirika makubwa ya Marekani.' Kwa mujibu wa Corbyn, tayari yameshafanyika mazungumzo juu ya suala hilo kati ya serikali ya Johnson na maafisa wa masuala ya biashara wa Marekani. Jeremy Corbyn amesema: "Tunachoelewa kuhusu mpango wa serikali-kutokana na kile ambacho Johnson amekifanya-ni vikao vya siri alivyofanya na Marekani; na katika vikao hivyo imependekezwa kuwa soko la mfumo wetu wa Huduma ya Taifa ya Afya lifunguliwe kwa ajili ya mashirika ya Kimarekani."  Kwa upande wake, Johnson amekanusha tuhuma hizo akisema "sio sahihi hata chembe", huku akisisitiza kwamba, mfumo wa Huduma ya Taifa ya Afya wa Uingereza katu hautauzwa.

Rais Donald Trump wa Marekani (kulia) na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson

Tuhuma mpya za Corbyn dhidi ya Johnson zimetokana na uungaji mkono wa kila hali wa Trump kwa Waziri Mkuu mhafidhina wa Uingereza, sambamba na ahadi chungu nzima alizotoa za kupanua na kustawisha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi baina ya nchi mbili baada ya kutekelezwa mpango wa Brexit, wa kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya. Marekani ina matumaini kuwa baada ya Uingereza kujitenga na Umoja wa Ulaya, soko la nchi hiyo litafunguliwa na kuwekwa wazi kwa ajili yake, ukijumuishwa mpango wa Huduma ya Taifa ya Afya, ambao ni sekta muhimu sana kwa mtazamo wa kiuchumi na kifedha; na hivyo kuweza kujipatia faida nono kupitia mpango huo. Jeremy Corbyn anaelewa vyema uhusiano wa karibu uliopo baina ya Trump na Johnson na muelekeo wa chama cha Wahafidhina wa kuwa na karibu zaidi na Washington baada ya Brexit, ikiwemo kufunga mkataba wa biashara huru na Marekani. Trump amemuelezea Boris Johnson kuwa ni mtu "safi sana" na kudai kwamba: Corbyn ataielekeza upande mbaya sana Uingereza. 

Mustakabali wa uhusiano wa Uingereza na Marekani katika kipindi cha baada ya Brexit, hivi sasa umegeuzwa kuwa suala zito katika uhusiano wa London na Washington. Licha ya hamu inayoonyeshwa na Chama cha Wahafidhina ya kustawisha uhusiano na Marekani, chama cha Leba hakijaonyesha msimamo chanya juu ya suala hilo. Katika hotuba yake ya kwanza ya kampeni za uchaguzi aliyotoa mwanzoni mwa mwezi huu wa Novemba, Jeremy Corbyn alisisitiza kuwa: "Hatutamuuzia Donald Trump au mwekezaji yeyote wa Kimarekani mfumo wetu wa Huduma ya Taifa ya Afya. Kauli hiyo ya Corbyn inaashiria tamaa waliyonayo Wamarekani ya kuhodhi uchumi, biashara na sekta ya umma ya Uingereza baada ya nchi hiyo kujitoa Umoja wa Ulaya. Kwa mtazamo wa kiongozi huyo wa chama cha Leba, suala hilo ni sawa na kuingilia masuala ya ndani ya Uingereza na ni ishara ya muelekeo wa kibeberu inaofuata Washington. Katika kipindi cha mwaka mmoja sasa, Rais Donald Trump wa Marekani ameshadidisha muelekeo wa kuingilia masuala ya ndani ya Uingereza, ambapo mbali na kuunga mkono kwa njia ya moja kwa moja uwaziri mkuu wa Boris Johnson amethubutu hata kutoa miongozo ya amri na makatazo kuhusu mazingira na namna ya kutekelezwa mchakato wa Brexit, kitendo ambacho kimekosolewa vikali na Corbyn. Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa chama cha Leba, Trump anajaribu kutumia kila njia kuingilia uchaguzi wa Uingereza ili kuhakikisha Johnson anakuwa waziri mkuu tena. Rais huyo wa Marekani anadhani kwamba, akichaguliwa tena Boris Johnson kuwa waziri mkuu wa Uingereza ataonyesha utiifu kamili kwa amri zake, na kwa njia hiyo yeye Trump ataweza kufanikisha yale aliyoyadhamiria ikiwemo kuhodhiwa na mashirika ya Marekani mfumo wa Huduma ya Taifa ya Afya wa Uingereza.../  

Maoni