Nov 21, 2019 07:50 UTC
  • Uturuki katika muamala wa hila na ujanja wa kupora maliasili za Syria

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesema, amelikataa pendekezo la kugawana utajiri wa mafuta ya Syria lililotolewa na baadhi ya madola ya kigeni.

Bila kuashiria jina la nchi yoyote, Erdoğan, ambaye alikuwa akihutubia mjini Istanbul, amesema: Baadhi ya madola ya kigeni yanataka mafuta ya Syria yagawanywe.

Lakini pamoja na madai hayo, Rais wa Uturuki amedai pia kwamba: Uturuki haifuatilii kupata mafuta ya Syria, bali lengo pekee inalofuatilia ni kuwasaidia wananchi wa nchi hiyo.

Marais wa Uturuki na Syria na familia zao enzi za uhusiano mzuri uliokuwepo kati ya nchi mbili

Matamshi hayo ya karibuni ya Rais wa Uturuki yametolewa, ilhali hakuna nchi yoyote iliyotoa kauli ya kuzungumzia suala la kugawanywa mafuta ya Syria. Marekani, ambayo ni nchi ya kibeberu yenye rekodi ndefu ya kuvamia na kukalia kwa mabavu ardhi za nchi zingine, hivi karibuni ilitangaza kuwa inayatumia na kuyauza mafuta ya Syria kwa ajili ya kufidia gharama za mahitaji ya wanamgambo wa Kikurdi wa nchi hiyo.

Kuhusiana na suala hilo inapasa tuseme kuwa: Serikali ya Marekani inataka kuimarisha satua na ushawishi wake katika maeneo yenye mafuta ya kaskazini mwa Syria hususan eneo la  Deir ez-Zur, ambapo hivi karibuni imeanzisha vituo kadhaa vya kijeshi katika maeneo hayo.

Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye sambamba na kuanza uvamizi wa kijeshi wa Uturuki kaskazini mwa Syria, alikuwa ameshatoa amri ya kuondoka wanajeshi wa Marekani katika eneo hilo, wiki kadhaa baadaye aliagiza idadi kadhaa ya askari wa Marekani waendelee kusalia nchini Syria kwa kisingizio cha kulinda visima vya mafuta ya nchi hiyo.

Wanajeshi wa Marekani wakiwa katika ardhi ya Syria

Pamoja na hayo, hadi sasa, si Marekani wala nchi nyingine yoyote ambayo imezungumzia suala la kutaka kupora na kutumia kwa ushirika na Uturuki vyanzo vya mafuta ya Syria. Kwa sababu hiyo, inaonekana kwamba, rais wa Uturuki amepitikiwa akilini mwake na ndoto ya kupora na kutumia vyanzo vya mafuta ya Syria kwa msaada wa Marekani.

Kwa matamshi aliyotoa hivi karibuni mjini Istanbul, Erdoğan ametuma salamu na ujumbe wa wazi kwa Marekani wa kuitaka ilitafakari wazo la kushirikiana na Uturuki katika wizi na uporaji wa mafuta ya wananchi wa Syria. Rais wa Uturuki anaota ndoto hiyo wakati Rais Bashar al-Assad wa Syria alisisitiza katika kauli aliyotoa mwezi uliopita wa Oktoba, kuhusu ulazima wa vikosi vya majeshi ya kigeni kuondoka katika ardhi ya nchi hiyo. Rais wa Syria alisema:

"Kulingana na sheria na mikataba ya kimataifa, vikosi vya majeshi ya Uturuki na Marekani, vinatambulika kuwa ni wavamizi; na wananchi wa Syria wana haki ya kupambana kukabiliana navyo."

Faisal al-Miqdad, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ambaye alikuweko nchini Oman kuhudhuria maadhimisho ya mwaka wa 49 wa Siku ya Taifa ya nchi hiyo, alizungumza pembeni ya sherehe hizo kuhusu mafanikio na ushindi liliopata jeshi la Syria katika kupambana na wavamizi na wezi wa mafuta ya nchi hiyo na kubainisha kwamba:

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Faisal al-Miqdad

"Taifa la Syria linawavizia maadui wote. Maliasili za nishati za Syria hazijahalalishwa kwa kila atakaye; na wakati mwafaka ukiwadia tutasimama kuzilinda. Syria ni nchi ya Wasyria wote na wala haifai kuipatia Uturuki kisingizio chochote kile kwa ajili ya kushambulia ardhi ya Syria."

Matamshi yote hayo yaliyotolewa na viongozi wa serikali halali ya Syria yanaonyesha kuwa, utumiaji wa aina yoyote wa rasilimali ya mafuta ya nchi hiyo unahesabiwa kuwa ni wizi na uporaji; na ni jambo la kushangaza kwa nchi kama Uturuki ambayo imekuwa kila mara ikidai kuwa inaunga mkono umoja wa Wasyria na ardhi yote ya nchi hiyo, kuona vipi inaridhia matakwa haramu ya maadui wa mataifa ya Waislamu.

Kuhusiana na nukta hiyo, kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Uturuki cha Jamhuri ya Watu, Kemal Kılıçdaroğlu, amesema, serikali ya Erdoğan haijapata funzo la kuzingatia kutokana na ilivyoshindwa nchini Syria na akatanabahisha kwamba:

"Ni kwa njia ya kufikia maridhiano tu na serikali ya Syria, ndipo serikali ya Uturuki itaweza kusalimika na shari ya ugaidi".

Kutokana na yote hayo inapasa tuseme kuwa: Siasa na sera mbovu za serikali ya Erdoğan zinatekelezwa nchini Syria, huku mustakabali wa uhusiano wa Uturuki na Syria ukiwa hauwezi kutabirika. Licha ya hatua kadhaa ilizopiga serikali ya Ankara katika masuala ya Syria ni vigumu kutasawari nini utakuwa mustakabali na hatima ya serikali ya Erdoğan katika masuala hayo.../

Tags

Maoni