Nov 25, 2019 02:52 UTC
  • Jumuiya za kimataifa zapinga uteuzi wa Ghada Wali kuwa Mkurugenzi wa UNODC

Jumuiya za kimataifa za kutetea haki za binadamu zimepinga uteuzi uliofanywa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na kumtangaza Ghada Wali, Waziri wa Ustawi za Jamii wa Misri kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Mihadarati na Jinai (UNODC).

Jumuiya hizo zimesema kuwa, Ghada Wali ameshiriki katika kukandamiza taasisi za kiraia kama zile za kutetea haki za binadamu na kutoa vitisho vya kuziadhibu tangu alipoteuliwa kuwa waziri mwaka 2014.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetangaza kuwa, kuchaguliwa Misri kwa ajili ya kushiriki katika mapambano dhidi ya mihadarati na uhalifu kutaipa nchi hiyo fursa ya kufuta sheria zinazohami na kutetea haki za binadamu hasa ikitiliwa maanani faili jeusi la nchi hiyo la ukiukaji mkubwa na wa kutisha wa haki za binadamu.

Mshauri wa masuala ya sheria wa Amnesty International, Simon Crowther amesema kuwa, hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa itakuwa na matokeo mabaya kwa haki za binadamau. Crowther ameongeza kuwa, serikali ya Misri inatumia mamlaka ya kupambana na ugaidi kwa ajili ya kukandamiza maelfu ya wapinzani wa kisiasa, kuwapoteza, kuwatesa na kukandamiza watetezi wa haki za binadamu.

Jela za Misri zimejaa wapinzani wa Abdel Fattah al Sisi

Ripoti iliyotayarishwa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kwa kushirikiana na Kituo cha Shihab na tasisi ya Uadilifu kwa Ajili ya Haki za Binadamu pia imesema idadi ya watu waliopotezwa na kutoweka imefikia 5500 na kwamba idadi ya vituo vya kushikilia watuhumiwa haijulikani nchini Misri.

Mwanasheria Toby Cadman wa taasisi ya Guernica 37 ya kutetea haki za binadamu yenye makao yake London nchini Uingereza amesema kuwa, takwimu zinazohusiana na hali mbaya ya haki za binadamu nchini Misri zinatisha hususan baada ya Abdel Fattah al Sisi kushika madaraka ya kuongoza nchi hiyo.

Cadman amesisitiza kuwa Abdel Fattah al Sisi anaendeleza ukatili na mauaji dhidi ya wapinzani na wakosoaji wake kwa himaya na uungaji mkono wa Rais Donald Trump wa Marekani na utawala wa Saudi Arabia.   

Tags

Maoni